Nuru FM

Bandari ya Dar es Salaam yaweka rekodi ikipokea magari 4,300

10 May 2022, 7:47 am

Meli kubwa ya shehena ya magari yapatayo 4,397 imewasili katika Bandari ya Dar es Salaam na kuvunja rekodi, ikiwa na idadi kubwa ya magari kuwasili kwa mara moja katika bandari hiyo.

Kaimu Mkurugenzi wa Masoko na Uhusiano wa TPA, Nicodemas Mushi amesema wanayofuraha kubwa kuipokea meli ya Meridian ACE, iliyovunja rekodi ya nyuma iliyowekwa mwezi mmoja uliopita ya kuwasili magari 4041 mwezi Aprili 8, 2022.

Meli hiyo imetokea nchini Japan na kupitia nchini Singapore na kuja moja kwa moja katika Bandari ya Dar es Salaam ambapo magari 991, yatabaki nchini Tanzania na magari 3,046 yatakwenda Zambia, Malawi, Rwanda, Burundi na DR Congo.

Aidha, amesema kuwasili kwa meli hiyo kuna maana kubwa katika uchumi wa Tanzania, kwani ujio wa meli kubwa kama Meridian Ace ni ishara ya ufanisi mkubwa wa Bandari ya Dar es Salaam, na pia ili kupata makampuni makubwa na mawakala wakubwa wenye mzigo kama huo ni lazima pawepo na imani ya watumiaji wa bandari.