Nuru FM

Iringa yaunda kamati kutatua changamoto za machinga

5 March 2024, 8:57 am

Kikao Cha Machinga na Kamati ya ulinzi na usalama Mkoa wa iringa. Picha na Hafidh Ally

Na Hafidh Ally

Mkoa wa Iringa umeunda kamati ndogo itakayofanya kazi siku saba kushughulikia ombi la wafanyabiashara wadogo maarufu wamachinga la kuwaruhusu wanawake kufanya shughuli zao katika eneo la mashine tatu muda wa jioni.

Mkuu wa mkoa huo Halima Dendego ametoa uamuzi huo kwenye kikao cha usuluhishi kati ya wamachinga na viongozi wa serikali wa wilaya na mkoa huo wenye lengo la kutafuta mwaroabini wa kudumu wa sakata la wamachinga.

Kikao hicho cha usuluhishi ni utekelezaji wa agizo la Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi Taifa, Paul Makonda aliyezuru mkoa huo hivi karibuni na kubaini mtifuano mkubwa kati ya serikali na wamachinga huku wamachinga wenyewe wakigawanyika makundi mawili ya SHIUMA na Machinga Network.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa Halima Dendego

Wamachinga waliofurika katika Ukumbi wa ofisi ya mkoa wa Iringa, wamesema chanzo cha vurugu ni chuki binafsi za viongozi wa makundi yao mawili kwa maslahi yao na kutaka wasigombee kuongoza tena.

Aidha wamachinga wanawake walimuomba Mkuu wa mkoa kuruhusu wafanya biashara mda wa jioni katika eneo la mashine tatu na Mkuu wa mkoa kuunda Kamati ya urataibu wa kufanya shughuli hizo.