Nuru FM

Malori yanayotoka Mufindi yakwama Nyamande

4 April 2024, 8:13 pm

Picha ikionesha Malori yalivyokwama.

Na Mwandishi wetu

Zaidi ya maroli 25 ambayo yanasafirisha bidhaa mbalimbali kutoka kiwanda cha karatasi Mgololo wilaya Mufindi mkoani Iringa yamekwamba kwa zaidi ya siku tano katika kijiji cha Nyamande na Kitandiliko halmashauri ya mji wa Makambako wilayani Njombe kutokana na ubovu wa barabara katika eneo hilo.

Wakizungumza na Nuru Fm baadhi ya madereva wa magari hayo wamesema changamoto kubwa katika eneo hilo ni wakala wa barabara kuweka kifusi chenye tope na kusababisha magari kukwama hasa katika kipindi hiki ambacho mvua inanyesha huku wakiishauri serikali kutengeneza barabara hiyo kwa kiwango cha lami ama changarawe.

Sauti ya Madereva wa Malori

Nao baadhi ya wananchi wa kijiji cha Kitandililo akiwemo wamesema kutokana na barabara hiyo kutopitaka kwa zaidi ya siku tano kumesababisha abiria wanaotoka mufindi kuishia kitandililo na kutafuta  gari lingine huku wanaotoka Makambako wakiishia Nyamande,ambapo wanalazimika kutembea umbari wa kilomita moja kuyafikia magari hayo.

Sauti ya Wananchi

Awali Diwani wa kata ya kitandililo Imani Fute amekiri kutokea kwa changamoto hiyo na kueleza kuwa barabara hiyo ipo chini ya wakala wa barabara (Tanroad) Iringa na kufafanua jitihada za kutatua adha hiyo zinaendelea kwa kuwasiliana na viongozi wa wakala wa barabara na mbunge wa jimbo la mufindi.

Sauti ya Diwani Fute

Naye meneja wa Tanroad mkoa wa Iringa Yudas Msangi amekiri kupokea changamoto hiyo na kueleza kuwa hali hiyo imesababishwa na mvua ambazo zinaendelea kunyesha na kufafanua kuwa wataifanyia marekebisho pindi mvua zikipungua huku akiweka mpango wa kuifanyia usanifu barabara hiyo na kuiombea fedha ili ijengwa kwa ikiwango cha lami.

Sauti ya Meneja wa Tanroad Iringa