Ndiwili kunufaika na ujenzi wa Zahanati
3 July 2026, 09:11

Na Hafidh Ally
Wananchi wa Kijiji cha Ndiwili, Kata ya Magulilwa wilayani Iringa, wanatarajia kuondokana na adha ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya, kufuatia ujenzi wa zahanati ya kijiji hicho kufikia hatua nzuri ya utekelezaji.
Akikagua maendeleo ya ujenzi huo katika siku ya kwanza ya ziara yake ya kikazi katika Jimbo la Kalenga mkoani Iringa, Mbunge wa Jimbo hilo, Jackson Kiswaga, amesema mradi huo unatekelezwa kwa ushirikiano kati ya Serikali, wananchi na Mfuko wa Jimbo la Kalenga. Amesema Serikali tayari imetoa shilingi milioni 60 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo.
Kiswaga amesema kukamilika kwa zahanati hiyo kutarahisisha upatikanaji wa huduma za afya kwa wakazi wa eneo hilo, hususan wanawake wajawazito, watoto na makundi mengine yenye uhitaji mkubwa wa huduma za matibabu, ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakilazimika kusafiri umbali mrefu kufuata huduma hizo.

Kwa upande wao, viongozi na wananchi wa Kijiji cha Ndiwili wamesema kukamilika kwa zahanati hiyo kutaboresha upatikanaji wa huduma za afya na kupunguza changamoto ya kusafiri umbali mrefu kwenda kupata matibabu.
Mradi huo unatekelezwa kwa fedha kutoka Serikali na Mfuko wa Jimbo la Kalenga, huku zaidi ya shilingi milioni nane zikihitajika ili kukamilisha ujenzi wa zahanati hiyo na kuanza kutoa huduma kwa wananchi.