Nuru FM

Baraza la Wazee laipongeza Iringa kwa kudhibiti ukatili

29 July 2026, 09:50

Baraza la Ushauri la Wazee Mkoa wa Iringa wakiwa kna Mkuu wa Mkoa wa Iringa Kheri James katika picha ya pamoja. Picha na Hafidh Ally

Viongozi hao wametoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na vyombo husika kutoa taarifa mapema kuhusu vitendo vya ukatili.

Na Hafidh Ally

Baraza la Ushauri la Wazee Mkoa wa Iringa limesema mkoa huo unaendelea kushuhudia mafanikio katika mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto, kufuatia kupungua kwa matukio hayo ikilinganishwa na miaka ya nyuma.

Baraza hilo limesema mafanikio hayo yametokana na utekelezaji wa mikakati mbalimbali inayoshirikisha Serikali, wadau wa maendeleo, viongozi wa dini na kimila pamoja na wananchi, huku utoaji wa elimu kuhusu madhara ya ukatili ukitajwa kuongeza uelewa wa jamii na kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika kuzuia na kutoa taarifa za vitendo hivyo.

Wakizungumza katika kikao chao na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, wajumbe wa Baraza la Ushauri la Wazee wamesema ushirikiano kati ya jamii na taasisi zinazoshughulikia ustawi wa jamii umechangia kupunguza vitendo vya ukatili huku wakisisitiza umuhimu wa kuendelea kutoa elimu kwa umma ili kuhakikisha matukio hayo yanazidi kupungua.

Sauti ya Wazee

Kwa upande wake, Afisa Ustawi wa Jamii katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Asheli Mndalila, amesema mafanikio hayo yametokana na ushirikiano wa karibu kati ya Serikali na wadau katika kutoa elimu kwa jamii, kuimarisha mifumo ya ulinzi wa watoto na kuhakikisha waathirika wanapatiwa huduma stahiki, huku hatua za kisheria zikichukuliwa dhidi ya watuhumiwa wa vitendo vya ukatili.

Sauti ya Afisa Ustawi

Naye Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, amewataka wananchi kuendelea kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya ukatili kwa kutovumilia vitendo hivyo, kutoa taarifa kwa wakati kwa mamlaka husika na kushirikiana na vyombo vya dola ili kuendelea kujenga mazingira salama kwa wanawake, watoto na makundi mengine ya jamii.

Sauti ya RC Kheri

Aidha,Mhe. Kheri amewataka wazee kuendelea kushirikiana na Serikali katika kukabiliana na changamoto zinazoikabili jamii, zikiwemo mmomonyoko wa maadili, ukatili dhidi ya watoto, wanawake na wazee pamoja na kuimarisha malezi ya vijana.