Nuru FM

Iringa yapongezwa kwa utekelezaji wa afua za afya

16 September 2026, 10:05

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Kheri James akizungumza na Maafisa Afya na usafi wa mazingira Mkoani Iringa. Picha na Hafidh Ally

Mafanikio hayo yanaonesha kuwa Mkoa wa Iringa una maafisa afya wenye uwezo, wanaowajibika na kujituma katika kutekeleza majukumu yao.

Na Hafidh Ally

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Kheri James, amewapongeza maafisa afya mkoani humo kwa utendaji mzuri unaochangia mkoa huo kufanya vizuri kitaifa katika utekelezaji wa afua za afya na usafi wa mazingira.

Mhe. Kheri ametoa pongezi hizo wakati akifungua Kikao cha Tathmini ya Utekelezaji wa Afua za Afya na Usafi wa Mazingira kwa mwaka 2025/2026, kilichofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa akisema mafanikio hayo yanaonesha kuwa wana maafisa afya wenye uwezo, wanaowajibika na kujituma katika kutekeleza majukumu yao.

Sauti ya RC Kheri

Mhe. Kheri amesema hadi kufikia Juni 2026, jumla ya vituo vya afya 170 pamoja na shule za msingi 282 vimeboresha miundombinu ya maji, usafi wa mazingira na usafi binafsi.

Sauti ya RC Kheri

Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Silvia Mamkwe, amesema mkoa huo umeendelea kufanya vizuri katika eneo la usafi wa mazingira, huku asilimia 98 ya kaya zikiwa na vyoo bora, hali inayoufanya Mkoa wa Iringa kuongoza kitaifa katika eneo hilo.

Sauti ya Mamkwe

Akizungumzia mikakati ya kuhakikisha mafanikio hayo yanaendelea, Afisa Afya wa Mkoa wa Iringa, Bi. Khadija Haroun, amesema miongoni mwa mikakati hiyo ni kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kuzingatia usafi na afya ya mazingira sambamba na kuwa na sheria na kanuni zinazotungwa na jamii katika ngazi za vijiji ili kuimarisha uwajibikaji na kuhakikisha usafi unakuwa sehemu ya maisha ya kila siku.

Sauti ya Khadija

Naye Kaimu Mkurugenzi kutoka Wizara ya Afya, Joseph Bilango, amepongeza Mkoa wa Iringa kwa hatua ulizopiga katika utekelezaji wa afua za afya na usafi wa mazingira akisisitiza umuhimu wa kuendelea kwa ushirikiano kati ya serikali, wataalamu wa afya na wananchi ili kudumisha mafanikio yaliyopatikana.

Sauti ya Bilango

Kikao hicho cha siku mbili kimewakutanisha wadau wa afya na usafi wa mazingira kwa lengo la kutathmini utekelezaji wa afua hizo na kuweka mikakati ya kuendelea kuboresha huduma za afya na usafi wa mazingira mkoani Iringa.