Nuru FM

Mikopo umiza yatishia ndoa Mafinga

23 August 2026, 09:06

Mbunge wa Jimbo la Mafinga akisikiliza kero za wananchi wa Kata ya Boma. Picha na Fredrick Siwale

Baadhi ya wanawake wanaodaiwa mikopo hiyo kukimbia na kuziacha ndoa zao kutokana na shinikizo linalotokana na wadai.

Na Fredick Siwale

Wananchi wa Kata ya Boma, Halmashauri ya Mji Mafinga, wametakiwa kujiepusha na mikopo inayotolewa na taasisi zisizosajiliwa, ikielezwa kuwa imekuwa chanzo cha migogoro ya kifamilia na kuvuruga ndoa.

Wito huo umetolewa na Diwani wa Kata ya Boma, Baraka Kisakanike, wakati wa ziara ya kikazi ya Mbunge wa Jimbo la Mafinga Mjini, Dickson Lutevele Villa.

Kisakanike amesema baadhi ya taasisi zinazotoa mikopo hiyo zimekuwa zikiwafuatilia wadaiwa hadi majumbani kwao, wakati mwingine nyakati za usiku, jambo ambalo amesema limekuwa likisababisha taharuki na migogoro katika familia.

Sauti ya Diwani Kisakanike

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Mafinga Mjini, Dickson Lutevele Villa, amesema Serikali imeweka mifumo ya kuwawezesha wananchi kupata mikopo yenye masharti nafuu, ikiwamo mikopo yenye riba ya asilimia 10, kwa lengo la kuwasaidia kujikwamua kiuchumi.

Villa amesema wananchi wanapaswa kutumia fursa hizo badala ya kukimbilia mikopo kutoka taasisi zisizosajiliwa ambayo inaweza kuwaongezea mzigo wa madeni.

Aidha, amezitaka benki kuweka masharti rafiki kwa wananchi, akisema riba ya asilimia 18 inayotozwa kwenye baadhi ya mikopo inaweza kuwa mzigo kwa wakopaji na kusababisha kushindwa kurejesha madeni yao kwa wakati.

Sauti ya Mbunge Villa

Katika ziata hiyo wananchi waliwasilisha kero zao ikiwemo changamoto ya barabara na maji ambapo Mbunge Villa amesema kuwa serikali itaendelea kutatua changamoto zote mara baada ya Bajeti kufika.