RC Kheri aitaka Mafinga kukamilisha kituo cha afya Wambi
29 September 2026, 08:58

Kituo hicho kitasaidia kuokoa maisha ya wananchi ambao kwa muda mrefu walilazimika kusafiri umbali mrefu kutafuta huduma za afya.
Na Chacha Robert
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, ameagiza Halmashauri ya Mji Mafinga kuhakikisha ujenzi wa Kituo cha Afya Wambi, kilichopo Kata ya Wambi, Wilaya ya Mufindi, unakamilika kwa wakati ili kuanza kutoa huduma kwa wananchi.
Kheri ametoa agizo hilo wakati wa ziara ya kikazi katika Halmashauri ya Mji Mafinga, baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho kinachojengwa kwa gharama ya Sh milioni 305.87, fedha zilizotolewa na Serikali Kuu mwezi Julai mwaka huu.
Akizungumza baada ya kukagua mradi huo, Kheri amewapongeza wananchi kwa kutenga eneo kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho, pamoja na uongozi wa Halmashauri na wataalamu kwa kuanza utekelezaji wa mradi kwa wakati.

Mkuu huyo wa Mkoa amesema Serikali inaendelea kuimarisha huduma za afya kwa wananchi kupitia ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya afya, akieleza kuwa baada ya kukamilika kwa jengo hilo, hatua inayofuata ni kuhakikisha kituo hicho kinapatiwa vifaa tiba na watumishi ili kiweze kuanza kutoa huduma.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Wambi, Mwinjilisti Frank Kalinga, amesema kwa muda mrefu kata hiyo haikuwa na kituo cha afya, hivyo ujenzi wa kituo hicho ni hatua muhimu katika kuboresha huduma za afya kwa wananchi.
Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Mtangani, Exavery Wita, amesema wananchi wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya kusafiri umbali mrefu kutafuta huduma za matibabu, akisema kukamilika kwa kituo hicho kutasaidia kusogeza huduma za afya karibu na wananchi na kupunguza adha ya kusafiri umbali mrefu.

Kwa mujibu wa Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya, Matilda Yassin, ujenzi wa kituo hicho unagharimu zaidi ya Sh milioni 300 na unalenga kuboresha huduma za afya kwa wananchi.
Amesema kituo hicho kitakuwa na jengo la huduma za wagonjwa wa nje pamoja na maabara, ambazo zitasaidia kuongeza upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi wa eneo hilo.
