Kilio cha wanafunzi Kidika kufuata shule mbali chakoma
1 October 2026, 12:11

Ujenzi wa shule hiyo unalenga kusogeza huduma ya elimu karibu na wananchi, pamoja na kupunguza hatari zinazoweza kuwakabili wanafunzi wanapokwenda na kurudi shuleni.
Na Chacha Robert
Kutokana na kuwepo kwa ajali zilizokuwa zikiwahusisha wanafunzi waliolazimika kutembea umbali mrefu kufuata elimu, Serikali imejenga Shule ya Awali na Msingi Kidika, iliyopo katika Kata ya Ruaha Mbuyuni, Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo, Mkoa wa Iringa.
Akisoma taarifa ya shule hiyo, Mwalimu Mkuu, Justine Mgina, amesema ujenzi wa mradi huo umegharimu zaidi ya shilingi milioni 284, huku ukiwa na lengo la kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia kwa wanafunzi wa eneo hilo.
Mwalimu Mgina amesema uwepo wa shule hiyo utasaidia kupunguza changamoto ya wanafunzi kutembea umbali mrefu kufuata elimu, hali ambayo hapo awali ilikuwa ikihatarisha usalama wao kutokana na ajali zilizokuwa zikitokea njiani.

Kwa upande wao, wananchi wa Kata ya Ruaha Mbuyuni wameishukuru Serikali kwa kujenga shule hiyo, wakieleza kuwa awali watoto wao walilazimika kutembea umbali mrefu kwenda shuleni, jambo ambalo lilisababisha baadhi yao kupata ajali na wengine kupoteza maisha.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa shule hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Kheri James, amesema shule hiyo imejengwa kwa viwango vya kisasa na itawapa wanafunzi mazingira bora ya kujifunza.
Mhe. Kheri amesema Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuboresha mazingira ya elimu nchini, huku akiwataka wananchi kutunza na kulinda miundombinu ya shule hiyo ili iweze kudumu na kunufaisha vizazi vijavyo.
Aidha, amewataka wazazi na walezi kuhakikisha wanawapeleka watoto wao shule ili wapate elimu itakayowawezesha kujenga maisha bora ya baadaye.
