Nuru FM

Tarura kuboresha miundombinu ya barabara na madaraja Kilolo

20 September 2026, 12:40

Mbunge wa Jimbo la Kilolo Dkt. Ritta Kabati akizungumza na Meneja wa Tarura Wilaya ya Kilolo Bw. Kidola. Picha na Hafidh Ally

Na Hafidh Ally

Mbunge wa Jimbo la Kilolo, Dkt. Ritta Enespher Kabati, amesema Serikali inaendelea kuboresha miundombinu ya barabara na madaraja ili kurahisisha shughuli za kiuchumi na kijamii kwa wananchi.

Dkt. Kabati ameyasema hayo wakati wa ziara ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo katika vijiji vya Winome na Mawambala, vilivyopo Kata ya Ukumbi, ambapo amesema hatua hiyo inalenga kuhakikisha barabara korofi zinapitika, hususan wakati wa msimu wa mvua.

Aidha, Dkt. Kabati ametembelea kivuko kinachounganisha Kijiji cha Winome na maeneo ya Iringa Vijijini, na kusema atashirikiana na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kuhakikisha changamoto hiyo inatatuliwa ili wananchi waweze kutumia njia hiyo bila kero.

Sauti ya Mbunge Kabati

Naye Meneja wa TARURA Wilaya ya Kilolo, Mhandisi Nkanda Jeremiah Kidola, amesema barabara korofi katika Kata ya Ukumbi zimewekwa kwenye mpango wa ukarabati, ikiwemo barabara na daraja linalounganisha Winome na Iringa Vijijini, ambalo linatarajiwa kujengwa kwa kiwango cha daraja la mawe Kwa gharama ya shilingi million 450.

Sauti ya Meneja Tarura Kidola

Aidha Mhandisi Kidola amesema wakati Tarura wakiendelea kufanya ukarabati wa miundombinu ya Barabara na madaraja, ni vyema wananchi wakachukua tahadhari Dhidi ya mvua za El-nino ambazo zinatarajiwa kuleta madhara katika makazi ya watu Kwa kuzibua mitaro na kusafisha mifereji.

Katika ziara hiyo, Dkt. Kabati pia amesikiliza kero mbalimbali za wananchi, ikiwemo changamoto za umeme, maji na miundombinu ya barabara, na kuahidi kushirikiana na mamlaka husika katika kuzitatua.

Daraja linalounganisha Kijiji cha Winome na Wilaya ya Iringa Vijijini linalotarajiwa kujengwa kwa Kiwango cha Mawe.