Nuru FM

ASAS akubali kuwa Mlezi wa Machinga

4 September 2023, 10:20 am

Salim Asas kutoka mkoani Iringa akipokea cheti cha Pongezi. Picha na Frank Leornard

Na Frank Leonard

MFANYABIASHARA Salim Asas kutoka mkoani Iringa  amekubali kupewa hadhi ya umachinga katika tukio lilikowenda sambamba na kuitikia wito wa kuwa mlezi na mwanachama wa Shirikisho la Umoja wa Machinga Tanzania (SHIUMA).

Katika tukio hilo lililofanyika katika soko la Machinga Mlandege mjini Iringa, Asas ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa Chama cha Mapinduzi (MNEC) amekabidhiwa kadi, barua ya ulezi, cheti cha pongezi na meza ya kuuzia bidhaa zake za maziwa katika soko hilo.

Hata hivyo meza hiyo pamoja na bidhaa zake aliitoa kwa uongozi wa machinga wilaya ya Iringa huku akiahidi kuwaongezea mtaji katika biashara hiyo ili faida watakayopata iwasaidie kugharamia shughuli mbalimbali za ofisi yao.

Katibu wa SHIUMA Taifa, Venatus Magayane alisema wamempa uanachama huo wakitambua kwamba Asas ni kiongozi wa biashara kubwa mwenye moyo usiochoka wa kutoa ushauri, usaidizi na mitaji kwa wafanyabiashara wadogo.

Akikubali maombi hayo, Asas ambaye tayari ametoa Sh Milioni 25 kati ya Sh Milioni 50 alizoahidi kwa machinga wa soko hilo kama mtaji watakaoutumia kukopeshana; alitumia tukio hilo kutoa darasa la biashara kwa wafanyabiashara hao.

Hata hivyo amesema changamoto kubwa inayowakabili wafanyabishara wadogo ni dhana waliyonayo ya kutengeneza fedha badala ya kukuza biashara zao.

Akiahidi kuendelea kuwasaidia wafanyabiashara hao, Asas amesema ni muhimu kwa machinga kukuza uhusiano wenye manufaa katika mazingira yanayoweza kusaidia biashara zao kustawi na kukua sambamba na biashara kubwa.

Katika tukio hilo, Asas ameahidi pia kujenga jengo maalumu kwa ajili ya huduma mbalimbali za watoto ambao mama zao wanafanyabiashara katika soko hilo lililojengwa kwa zaidi ya Sh Milioni 200 zilizotolewa na yeye mwenyewe.

Awali Mstahiki Meya wa Manispaa ya Iringa, Ibrahim Ngwada amesema halmashauri yao inazo Sh Milioni 10 zilizotolewa na Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya ujenzi wa ofisi ya machinga ya wilaya na kwamba mpango wao ni kuongeza fedha na kujenga ofisi kubwa zaidi.