Nuru FM

Madiwani Mafinga watoa tamko bei ya nyama

5 August 2023, 10:25 am

Mwenyekiti Wa Halmashauri Mafinga Mji Reginant Kivinge akizungumza katika Baraza la Madiwani Mjini Mafinga. Picha na Hafidh Ally

Na Hafidh Ally

Baraza la Madiwani halmashauri ya Mji wa Mafinga Mkoani Iringa limeridhia bei ya nyama iuzwe kwa shilingi elfu 9 baada ya wafanyabiashara wa nyama kuuza kwa shilingi elfu 10.

Hatua hiyo imekuja baada ya kuongezeka kwa bei ya nyama na kuzua taharuki kwa walaji ambapo awali nyama ilikuwa ikiuzwa kwa shilingi elfu 7 mpaka elfu 8 kwa kilo moja.

Akizungumza katika kikao cha baraza la madiwani kilichoketi kujadili Taarifa ya robo nne ya mwaka kuanzia April hadi june ya mwaka wa fedha 2022/2023 Mwenyekiti wa Halmashauri Mafinga Mji Reginant Kivinge amesema kuwa bei hiyo imetokana na kuadimika kwa ng’ombe.

Makamu Mwenyekiti wa wafanyabiashara wa nyama mafinga Mji Rashid Ng’umbi.

“sisi tumefanya utafiti na kubaini kuwa katika maeneo mengi hasa ya iringa mjini, makambako na kwingineko bei ya nyama ni shilingi elfu 9 kwa kilo, hivyo nawasihi wafanyabiashara walioamua kuuza nyama kwa shilingi elu 10 kwa kilo waache.” Alisema Kivinge

Kivinge amebainisha kuwa Bei ya nyama inatokana na uwepo wa soko huria ambalo linawalazimu wauzaji wapange bei kutokana na gharama za upatikanaji wa mifugo.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa wafanyabiashara wa nyama mafinga Mji Rashid Ng’umbi amebainisha kuwa sababu ya kupanda kwa bei ya nyama Mjini mafinga ni kutokana na kupanda kwa gharama za uendeshaji.

Aidha amesema kuwa kwa sasa wameshusha nyama kutoka elfu 10 mpaka elfu 9 kutokana na wateja kususa kununua kitoweo.

“Sisi tunafuata mifungo kutoka madibila, Rujewa, songwe ambapo baada ya wafugaji kutoka bonde la ihefu kuhamishwa na serikali ilipelekea sisi kuwafuata mifugo mbali na kupelekea kuadimika kwa mifigo na kuongezeka kwa gharama za uendeshaji’ alisema Ng’umbi

Kwa upande wao baadhi ya wauzaji wa chakula mjini mafinga wamesema kuwa kwa sasa wameamua kupandisha chakula kutoka shilingi 1,500 mpaka 2,500 kwa sahani moja ya wali kutokana na ongezeko la bei nyama.

MWISHO