Nuru FM

Wakwamishaji miradi Kigoma kukiona

21 May 2022, 11:16 am

Baraza la madiwani Halmashauri ya manispaa ya Kigoma Ujiji limeazimia kwa kauli moja kuchukulia hatua kwa viongozi wa wafanyabiashara wanaokwamisha mpango wa ujenzi na maboresho ya masoko ya Kigoma na Mwanga.

Akiwasilisha ajenda maalum ya kujadili ujenzi wa masoko hayo katika baraza la madiwani la Halmashauri ya manispaa ya Kigoma ujiji  Diwani wa kata ya Rusimbi Bakari Songoro amesema viongozi hao wa masoko wanafanya vibaya kuzuia mpango wa maendeleo.

“Kipindi cha nyuma mpango wa ujenzi ulikwama kwa sababu ya siasa za upinzanj lakini leo baraza lina madiwani 18 wa CCM na wa upinzani mmoja lakini uzuiaji wa mipango ya maendeleo unasababishwa na viongozi ndani ya chama kwahili hapana,” amefafanua Songoro.

Akiongea katika kikao hicho Mwenyekiti wa kamati ya mipango Miji Diwani wa kata ya Machinjioni manispaa ya Kigoma Ujiji Himid Omari ameshangazwa kukwama kwa ujenzi wa masoko hayo licha ya taratibu zote za kisheria kufanyika.

“kila kitu tayari ikiweo kuteua maeneo ya kuwahamishia wafanyabiashara kwa muda ili kupisha ujenzi na tayari timekaa na wafanyabiashara kuzungumzia hili wamekubali kuhama kupisha ujenzi sasa tatizo linatoka wapi?,” ameuliza Diwani Omary.

Naye Diwani kata ya Kasimbu Fuad Seif aliwataja baadhi ya viongozi wa masoko ya Mwanga na soko la kigoma kuongoza mpango wa kuzuia ujenzi wa masoko hayo kutokana na maslahi binafsi na kwamba mpango wa kuvunjwa na kujengwa upya kwa masoko hayo utawafanya kushindwa kukusanya mapato.

Kwa upande wake Diwani wa kata ya Rubuga (CHADEMA), Omari Gindi amelaani vitendo vinavyofanywa na baadhi ya wafanyabiashara wanaozuia mpango wa ujenzi wa masoko hayo kwa maslahi binafsi wakati mpango huo unalenga uboreshwaji na kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato.

“baadhi ya watu hapa Kigoma wamekuwa na tabia ya kuzuia miradi mfano mradi wa upanuzi wa uwanja wa ndege wa Kigoma hadi sasa umekwama licha ya pesa kuwepo jambo hili lisijirudie kwenye ujenzi wa masoko,” amesisitiza Gindi.

Mkuu wa wilaya Kigoma Esther Mahawe akiongea katika kikao hicho amesikitishwa na mpango wa kukwamisha ujenzi huo huku akisema tayari taratibu zote zimefanywa ikiwemo kukaa na wafanyabiashara hao kwa maridhiano ya pande mbili.

Awali Mwenyekiti wa CCM wilaya Kigoma Mjini Yassin Mtalikwa amesema kama chama hawakubaliani na mpango wa kukwamishwa kwa ujenzi wa masoko na watachukua hatua kupitia vikao kwani hatua hiyo inalenga kukwamisha utekelezaji wa ilani ya chama.

Akihitimisha Mjadala huo Meya wa Manispaa ya Kigoma, Baraka Naibuha amesema hatua stahiki zitachukuliwa kwa mujibu wa sheria na maamuzi ya kikao ili kuhakikisha hakuna mkwamo katika utekelezaji wa maendeleo ya wananchi.