Nuru FM

Wazazi watakiwa kufanikisha Mabaraza ya Watoto

11 September 2022, 3:33 pm

Rais, Samia Suluhu Hassan amewataka wazazi na walezi nchini, kuwaruhusu watoto wao kushiriki kwenye Mabaraza ya watoto yaliyopo katika ngazi za Kata hadi Taifa, ili kujenga vipaji vyao vinavyopatikana kwenye mabaraza hayo.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dorothy Gwajima ameyabainisha hayo wakati wa kumkabidhi Bendera ya Taifa, Mtoto Victor Paschal Tantau anayetarajiwa kushiriki Mkutano wa Jukwaa la Watoto Duniani utakaofanyika nchini Denmark Septemba 13 – 16, 2022.

Amesema, Watoto wana haki ya kushiriki na kushirikishwa kwenye masuala yanayowahusu, katika kutekeleza haki yao ya msingi nayotambuliwa na Baraza la Usalama la Umoja la Umoja wa Mataifa, likihusisha viongozi wa nchi wanachama uliofanyika Mei 8 – 10, 2002.

Waziri Gwajima, ameongeza kuwa, “Katika kutekeleza azimio hilo, Desemba 2002 Serikali iliunda Baraza la Watoto la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ili kuwezesha Watoto kukutana na kujadili masuala yanayohusu haki, ulinzi na maendeleo yao kwa ujumla.”

Aidha, amesema katika kuimarisha ushirikishwaji wa Watoto , Serikali imeandaa Sera ya Maendeleo ya Mtoto ya Mwaka 2008, na kwenye Sura ya 5 imetoa maelekezo kwa wadau kuhakikisha kuwa Watoto wanashirikishwa katika masuala yanayowahusu.

“Sheria ya Mtoto Namba 21 ya Mwaka 2009 inatambua kwamba mtoto anapaswa kushirikishwa masuala yanayomhusu” amesema Waziri Dkt. Gwajima