Nuru FM

Watoto watatu wa familia wateketea kwa moto

23 January 2023, 10:36 am

Watoto watatu wa familia ya BI Karesma Theodory wa wilaya ya Rombo Mkoani Kilimanjaro wamefariki dunia baada ya kuteketea kwa moto unaodhaniwa kusababishwa na Bibatari.

Tukio hilo lililoibua simanzi, lilitokea usiku kijijini humo kwa kile kinachodaiwa chanzo ni kibatari ambacho watoto walikuwa wakikichezea ndani ya nyumba yao.

Watoto hao waliofariki dunia kwa kuteketea kwa moto wakati mama yao akiwa ametoka nje akiongea na simu na mume anayeishi nchini Kenya ni Erick (9), Joshua (7) na Gidion Theodory (2).

Mkuu wa Wilaya ya Rombo, Kanali Hamis Maiga amethibitisha kutokea kwa tukio hilo akisema chanzo cha moto ni kibatari ambacho watoto hao walikuwa wakikichezea ndani wakati mama yao akiwa nje.

Miili ya watoto hao imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti Kituo cha Afya cha Karume kilichopo wilayani humo kwa ajili ya taratibu za maziko.