Nuru FM

Kamera kufungwa Majinja, Kitonga kudhibiti ajali

14 August 2023, 11:56 am

Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama Barabarani Salim Abri Asas Akizungumzia kuhusu uwekaji wa teknolojia ya kamera. Picha na Hafidh Ally

Na Hafidh Ally

Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama Barabarani Salim Abri Asas ameahidi kufunga kamera katika maeneo ya Majinja na Mlima Kitonga ili kuwabaini madereva ambao watashindwa kufuata sheria za usalama barabarani.

Salim Asas ameyasema hayo baada ya kamati ya usalama Barabarani Mkoa wa iringa kufanya ziara ya ukaguzi wa maeneo ambayo si salama kwa uendeshaji wa magari katika barabara ya TANZAM Iringa-Mbeya na kuongeza kuwa zoezi la ufungaji wa kamera litasaidia kupunguza ajali za barabarani.

“Tutatafuta wataalamu ambao watakuja kufanya usanifu katika eneo la majinga na kitonga ili tufunge kamera ambazo zitakuwa zinaonesha jinsi madereva watakavyopita na kuwabaini wale ambao watakiuka sheria za usalama barabarani” alisema Asas

Kamati ya Usalama Barabarani Mkoa wa Iringa.

Amesema kuwa kwa sasa teknolojia imekuwa hivyo kamati yao ya usalama imeona ni vyema kuziweka kwa kuwa polisi hawawezi kukaa muda wote katika eneo hilo kutokana na mazingira.

Kwa upande wake kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa ACP Allan Lucas Bukumbi amesema kuwa wameamua kuangalia barabara zote ambazo zimekuwa chanzo cha ajali ili kuangalia mifumo ya namna ya kudhibiti na kuokoa uhai wa watumiaji wa barabara.

Aidha amewataka madereva kufuata sheria za usalama barabarani hasa katika maeneo ambayo ni hatari ikiwemo eneo la Majinja na mlima Kitonga ili kuepukana na ajali.

Naye Mrakibu Mwandamizi wa Jeshi la Polisi Mossi Ndozero ambaye ni Mkuu wa usalama Barabarani Mkoa wa Iringa amewataka madereva kutii sheria na kanuni za usalama barabarani kwani askari wa usalama barabarani wako imara kuhakikisha usalama unakuwepo wakati wote.

“sisi tuko imara kuwachukulia hatua madereva ambao wanapita katika barabara hii wasiotii sheria, hivyo niwasihi pia abiria wawe wanatoa taarifa pindi wanapoona madereva wanaendesha magari bila kufuata sheria za barabarani” alisema Ndozero

Katika ziara hiyo Kamati ya ulinza na usalama barabarani iliwakamata madereva watatu ambao walikiuka sheria za usalama barabarani ambao ni Dereva wa Basi la Golden Deer Hashimu Jumanne Fonga na Dereva wa Basi la Kampuni ya Aboood Reniely Julias wanaofanya safari kutoka Dar es salaam kwenda Tunduma kwa kutofuata sheria za usalama barabarani pamoja na dereva wa basi la Ngasere High Clasic Joackim Mapunda lenye namba za usajili T 978 DWX.

MWISHO