Nuru FM

Dkt. Dugange: Udumavu bado tishio nchini

7 May 2024, 8:44 pm

Naibu Waziri Dugange katika picha ya pamoja jijini Dodoma. Picha na Mwandishi wetu

Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) anayeshughulikia Afya, Dkt. Festo Dugange amesema takwimu zinaonesha kuwa kiwango cha udumavu kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano bado ni kikubwa ambapo kwa mkoa wa Kigoma ni asilimia 27.1, Katavi asilimia 32.2, Njombe asilimia 50.4, Songwe asilimia 31.9 na Rukwa asilimia 49.8.

Amesema hayo katika hafla ya kusaini hati za makubaliano ya utekelezaji wa mradi wa lishe unaofadhiliwa na Shirika la Misaada la Watu wa Marekani (USAID) iliyofanyika leo Mei 07, 2024 katika Ukumbi wa Sokoine jijini Dodoma.

Dkt. Dugange amesema viwango vya matatizo ya lishe nchini vimeendelea kupungua mwaka hadi mwaka ambapo kwa mwaka 2022 kiwango cha udumavu nchini ni asilimia 30 ikilinganishwa na asilimali 34 mwaka 2015.

Aidha, Naibu Waziri huyo amesema jamii inapaswa kuendelea kuhamasisha ulaji wa chakula mchanganyiko chenye virutubisho na kuzingatia mtindo bora wa maisha.

“Tuweke kipaumbele katika kuimarisha usafi wa mazingira na kutokomeza imani na mila potofu zinazoathiri lishe,” amesema.

Aidha, amewataka viongozi katika mikoa na halmashauri kuzingatia na kudhibiti maradhi yanayochangia matatizo ya lishe na kuimarisha uhakika wa chakula na matunzo bora ya wanawake na watoto.

“Tukiyafanya haya yote kwa weledi na ufanisi wa hali ya juu program hii ya lishe inayozinduliwa leo itachangia kikamilifu na kuongeza kasi ya kupunguza udumavu na matatizo mengine ya lishe nchini,” amesema Dk Dugange.

Pia, ameahidi kuwa Ofisi ya Rais – TAMISEMI itatoa ushirikiano wa kutosha kwa wadau wote wa program ya lishe ili kuhakikisha kuwa malengo ya program hii yanafikiwa kwa manufaa ya wananchi wote kwa ujumla.

CHANZO: Habari Leo