Wananchi Ugute wakosa huduma ya maji mwezi mzima
25 July 2026, 16:54

Wananchi hao wameiomba Serikali kusogeza karibu vituo vya kuchotea maji ili kuwaondolea adha ya kutembea umbali mrefu kufuata maji, jambo ambalo limekuwa likiwaathiri zaidi wanawake na watoto.
Na Fredrick Siwale
Wananchi wa Kijiji cha Ugute, Kata ya Isalavanu katika Jimbo la Mafinga Mjini mkoani Iringa, wamelalamikia kukosekana kwa huduma ya maji kwa zaidi ya mwezi mmoja licha ya kijiji chao kupitiwa na mradi wa maji.
Wakizungumza wakati wa ziara ya kikazi ya Mbunge wa Jimbo la Mafinga Mjini, Mheshimiwa Dickson Lutevele Villa, wananchi hao walisema kuwa wakati wa utekelezaji wa Mradi wa Maji wa Ugute–Kitelewasi walipewa ahadi ya kufungiwa koki ya maji kwenye moja ya matanki yaliyopo kijijini hapo, lakini hadi sasa maji hayajatoka, hali inayowalazimu kuendelea kukosa huduma hiyo muhimu.
Akizungumzia changamoto ya maji, Kaimu Mhandisi wa RUWASA Wilaya ya Mufindi, Irene Sangiwa, alisema kituo cha Ugute kinakabiliwa na tatizo la upatikanaji wa maji kutokana na eneo hilo kuwa kwenye mteremko, hali inayosababisha maji kushindwa kufika kwa mtiririko wa kawaida.
Ameongeza kuwa RUWASA imepanga kufunga pampu za kusukuma maji ili kuhakikisha huduma hiyo inapatikana katika vituo vyote vinavyokabiliwa na changamoto hiyo.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Mafinga Mjini, Mheshimiwa Dickson Lutevele Villa, amesema ifikapo Agosti 24 mwaka huu wananchi wa Kijiji cha Ugute wanapaswa kuanza kupata huduma ya maji, baada ya RUWASA kukamilisha hatua za kutatua changamoto zilizosababisha kukosekana kwa huduma hiyo.