Nuru FM

Wamiliki wa Vituo vya watoto waungana kupeana maarifa

22 September 2026, 11:35

Wamiliki wa makao ya watoto na vituo vya malezi ya watoto (Day Care) Mkoa wa Iringa katika picha ya Pamoja. Picha na Adelphina Kutika

Umoja huo unawaunganisha wamiliki wa makao ya watoto nchini, ambao kwa sasa wanafikia takribani 500,  ili waweze kuwa na mfumo wa pamoja wa kushughulikia changamoto zinazowakabili katika kutoa huduma za malezi.

Na Adelphina Kutika

Wamiliki wa makao ya watoto na vituo vya malezi ya watoto (Day Care) Mkoa wa Iringa wamekutana kwa pamoja kwa lengo la kuzungumza kwa lugha moja, kubadilishana uzoefu wa malezi na makuzi ya watoto, pamoja na kuunda uongozi utakaosimamia umoja wao.

Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika katika Ukumbi wa Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mwenyekiti wa Umoja wa Wamiliki wa Makao ya Watoto Taifa, Evance Tegete, amesema lengo la kikao hicho ni kuwaunganisha wamiliki wa makao ya watoto, kubadilishana uzoefu kuhusu malezi na makuzi ya awali ya mtoto, pamoja na kujadili umuhimu wa kuwa na uongozi imara.

Sauti ya Mwenyekiti

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Umoja wa Wamiliki wa Makao ya Watoto Mkoa wa Iringa, Jane Hussen Mwalembe, aliyechaguliwa kuongoza umoja huo, amesema atahakikisha anawaunganisha wamiliki hao ili kuwa na umoja imara na unaoweza kuwasaidia kujitegemea kiuchumi.

Sauti ya Jane

Naye Mwenyekiti wa Day Care Mkoa wa Iringa, Fanikisha Peter, amesema moja ya changamoto kubwa inayojitokeza ni kuibuka kwa vituo vya malezi ya watoto vinavyoanzishwa bila waendeshaji kuwa na elimu na taaluma inayohitajika katika malezi ya watoto.

Sauti ya Fanikisha

Kwa upande wake, Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Iringa, Martine Chuwa, amewataka wamiliki wa makao ya watoto kuhakikisha wanatoa malezi na huduma zinazolenga ustawi wa mtoto badala ya kuishia kuwahifadhi watoto pekee.

Chuwa amewataka wamiliki hao kutumia wataalamu wa ustawi wa jamii waliopo katika kata zao pale wanapokutana na changamoto zinazohusu watoto, akisisitiza kuwa maafisa hao wana ujuzi wa kutoa ushauri na mwongozo kuhusu malezi na ustawi wa watoto.