Nuru FM

Uelewa wa maambukizi ya VVU waongezeka kwa 94.6% Iringa

18 November 2026, 09:19

Mkuu wa Mkoa wa Iringa Kheri James akipokea taarifa ya kuhusu uelewa wa maambukizi ya ukimwi kwa wananchi. Picha na Hafidh Ally

Na Hafidh Ally

Kiwango cha uelewa wa wananchi kuhusu maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) mkoani Iringa kimeongezeka kutoka asilimia 86.5 hadi asilimia 94.6 ndani ya kipindi cha miaka mitano, huku kiwango cha kitaifa kikiwa asilimia 95.

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Mradi wa Afya Yangu Southern Project, Dkt. Denis Mzaga, wakati wa hafla ya kukabidhi vitendea kazi baada ya mradi huo kumaliza muda wake wa utekelezaji.

Dkt. Mzaga amesema kuwa katika kipindi hicho, asilimia 98 ya watu waliobainika kuwa na maambukizi ya VVU wameanzishiwa matibabu, huku asilimia 98 ya wanaotumia dawa za kufubaza virusi hivyo wakifikia kiwango cha udhibiti wa virusi mwilini.

Amesema kuwa katika kipindi cha miaka mitano ya utekelezaji wa mradi huo, vituo 147 vya kutolea huduma za matibabu na ufuatiliaji wa VVU (CTC) vimekuwepo, huku jumla ya wananchi 71,149 wakinufaika na huduma za matibabu.

Hata hivyo, Dkt. Mzaga ametoa tahadhari kuhusu uwepo wa watu wanaopata maambukizi mapya ya VVU, akieleza kuwa baadhi yao wamebainika kuwa katika hatua ya ugonjwa, hali inayohitaji kuimarishwa kwa juhudi za kinga na upimaji wa afya.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Kheri James, amewataka Waganga Wakuu wa Halmashauri zote mkoani humo kuendelea kutoa elimu na kuhamasisha wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya maambukizi mapya ya VVU.

Mhe. James amesema Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo, wakiwemo Shirika la Misaada la Marekani (USAID), imefanya juhudi mbalimbali za kupunguza kasi ya maambukizi, hivyo ni wajibu wa wataalamu wa afya katika halmashauri kuendeleza juhudi hizo ili kufikia lengo la asilimia 95-95-95 ifikapo mwaka 2030.

Aidha, amesema vitendea kazi vilivyokabidhiwa na wadau wa mradi huo vinapaswa kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa ili kuendeleza huduma na mapambano dhidi ya VVU na Ukimwi mkoani Iringa.

Ameagiza pia Waganga Wakuu wa Halmashauri kufuatilia kwa karibu watu wanaobainika kuwa na maambukizi ya VVU ili kuhakikisha wanapata huduma na matibabu stahiki kwa wakati, pamoja na kuimarisha juhudi za kuzuia maambukizi mapya.