Simba avamia Maeneo ya Makazi Mufindi
20 August 2026, 21:46

Wananchi Mufindi Watakiwa Kuchukua Tahadhari Baada ya Simba Kuvamia Maeneo ya Makazi
Na Fredrick Siwale
Wananchi wa Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa wametakiwa kuchukua tahadhari kufuatia kuonekana kwa simba katika Kata ya Nyololo, ambaye amekuwa akivamia maeneo ya makazi na kula mifugo ya wananchi.
Akizungumza katika kikao cha Baraza la Madiwani cha Robo ya Nne, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi, Mheshimiwa Boniface Masangula, amesema wananchi wanapaswa kuwa makini, hususan wazazi na walezi, kutokana na uwepo wa simba huyo.
Amesema tahadhari zaidi inahitajika kwa wanafunzi wanaoamka mapema kwenda shuleni, akieleza kuwa simba huyo tayari amesababisha madhara kwa wananchi kwa kuwinda mifugo.

Kwa upande wake, Afisa Maliasili na Uhifadhi wa Mazingira wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi, Gilibert Ngailo, amethibitisha kuwepo kwa simba katika maeneo yanayokaliwa na wananchi na kusema kuwa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) inaendelea na jitihada za kumtafuta na kumdhibiti.
Ngailo amesema simba huyo tayari amesababisha hasara kwa wananchi, ambapo jumla ya ng’ombe wanane wameuliwa, sambamba na mbuzi na nguruwe.
Wananchi wametakiwa kuendelea kuchukua tahadhari na kutoa taarifa kwa mamlaka husika endapo watamuona simba huyo, ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa.