Nuru FM

Madaktari Mafinga wafukuzwa kazi kwa kuchati

27 August 2026, 09:12

Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mji Mafinga, Dkt. Victor Msafiri akizungumza na wananchi. Picha Fredrick Siwale

Wananchi wa Halmahauri ya Mji Mafinga wamelalamikia tabia ya wahudumu wa afya katika hospitali kuchati badala ya kuwahudumia.

Na Fredrick Siwale

Madaktari saba kutoka Halmashauri ya Mji Mafinga wamefukuzwa kazi, huku wengine wakipangiwa majukumu mengine, ikiwemo kushiriki katika zoezi la ukusanyaji wa taka kwa kutumia magari yanayopita mitaani, hatua inayolenga kudhibiti nidhamu na kuongeza weledi katika utoaji wa huduma za afya.

Akizungumza wakati wa ziara ya Mbunge wa Jimbo la Mafinga Mjini, Mheshimiwa Dickson Lutevele Villa, Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mji Mafinga, Dkt. Victor Msafiri, amesema hatua hizo zimechukuliwa baada ya kuwepo kwa malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu utolewaji duni wa huduma katika hospitali hiyo.

Amesema lengo la hatua hizo ni kuhakikisha watumishi wanazingatia maadili, nidhamu na weledi wakati wa kuwahudumia wagonjwa.

Sauti ya Victor

Dkt. Victor Msafiri amewataka wananchi wanaofika hospitalini kupata huduma za afya kutoa taarifa pindi wanapobaini mtumishi anashindwa kutekeleza majukumu yake, ikiwemo kutumia muda wa kazi kuchati badala ya kuwahudumia wagonjwa.

Amesema taarifa hizo zinaweza kuwasilishwa katika ofisi yake ili hatua za kinidhamu zichukuliwe dhidi ya watumishi watakaobainika kukiuka wajibu wao.

Sauti ya Victor

Akizungumzia mipango ya kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa wananchi wa Halmashauri ya Mji Mafinga, Mbunge wa Jimbo la Mafinga Mjini, Mheshimiwa Dickson Lutevele Villa, amesema amewasilisha maombi ya kupatiwa gari la kubebea wagonjwa (ambulance).

Mbunge huyo amesema gari hilo linatarajiwa kufika kati ya mwezi Septemba na Novemba mwaka huu.

Sauti ya Mbunge