Nuru FM

Wanafunzi waliofadhiliwa na Camfed watakiwa kung’ara masomoni

26 June 2026, 12:09

Wasichana waliochaguliwa kujiunga na elimu ya Kidato cha Tano kwa mwaka wa masomo 2026/2027 kupitia ufadhili wa Shirika la CAMFED katika picha ya pamoja. Picha na Adelphina Kutika

Wanafunzi hao wanapaswa kuitumia vyema fursa waliyoipata kwa kuongeza bidii na kujituma katika masomo yao ili kutimiza ndoto walizojiwekea na kuwa mfano bora kwa jamii.

Na Adelphina Kutika

Wasichana waliochaguliwa kujiunga na elimu ya Kidato cha Tano kwa mwaka wa masomo 2026/2027 kupitia ufadhili wa Shirika la CAMFED wametakiwa kuwa vinara wa masomo na maadili mema badala ya kujihusisha na tabia zisizofaa zinazoweza kuathiri maendeleo yao ya elimu na maisha ya baadaye.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Shule ya Sekondari Igowole, Innocent Mgoda, wakati akihitimisha Jukwaa la Wasichana la Kimkoa lililoandaliwa na Shirika la CAMFED katika Wilaya ya Mufindi, mkoani Iringa na kuongeza kuwa wanafunzi hao wanapaswa kuitumia vyema fursa waliyoipata kwa kuongeza bidii na kujituma katika masomo yao.

Sauti ya Mgoda

Kwa upande wake, Afisa Miradi wa Mkoa wa Iringa kutoka Shirika la Campaign for Female Education (CAMFED), Neema Msemwa, amesema jukwaa hilo limeandaliwa kwa lengo la kuwasaidia wasichana hao kutambua fursa na changamoto zinazoweza kuwakabili katika maisha yao ya sasa na ya baadaye ili waweze kupanga mikakati ya kufikia malengo yao.

Sauti ya Neema

Naye Muuguzi na Mkunga kutoka Kituo cha Afya Sadani, Hellena Adriliano Michael, amesema jukwaa hilo limewapa washiriki elimu ya afya ya uzazi, afya ya hedhi na namna ya kujikinga dhidi ya mimba za utotoni pamoja na magonjwa yanayoathiri afya ya uzazi.

Sauti ya Mkunga

Awali  Afisa Mauzo kutoka Benki ya NMB tawi la Mafinga, Anteline Kabera, amesema benki hiyo ilitumia fursa hiyo kutoa elimu ya fedha ikiwemo umuhimu wa kuweka akiba, kupanga matumizi na kujenga utamaduni wa kujitegemea kiuchumi tangu wakiwa shuleni huku wasichana hao wakishukru kwa kupewa elimu hiyo.

Sauti ya Kabera vs Wasichana

Jukwaa hilo la kimkoa limewakutanisha wasichana 400 kutoka halmashauri mbalimbali za Mkoa wa Iringa waliochaguliwa kujiunga na Kidato cha Tano katika mwaka wa masomo 2026/2027 Lengo likiwa ni kuwajengea uwezo wa kimaisha, kielimu na kijamii kabla ya kuanza safari yao ya elimu ya juu ya sekondari, sambamba na kuwapa nafasi ya kujifunza kutoka kwa wataalamu wa sekta mbalimbali.