Nuru FM
Nuru FM
5 May 2026, 19:42

Uboreshaji wa machinjio hayo utachochea maendeleo ya sekta ya mifugo pamoja na kuongeza thamani ya mazao ya mifugo mkoani Iringa.
Na Hafidh Ally
Zaidi ya Bilioni 1 zinataajia kuboresha machinjio ya Ngelewala yaliyopo Manispaa ya Iringa ikiwemo kununua mashine za kisasa ili kuongeza ufanisi na ubora wa huduma za uchinjaji nyama.
Hayo yamezungumzwa na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Iringa Mhe. Ibrahim Ngwada, katika kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo ambapo maboresho hayo ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa serikali wa kuinua viwango vya machinjio nchini na kuhakikisha wananchi wanapata nyama salama na yenye ubora unaokidhi viwango vya afya.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Mwangata Mhe. Galus Lugenge, amepongeza uwekezaji huo akisema utaondoa changamoto zilizokuwepo awali katika utoaji wa huduma za machinjio na hivyo kuimarisha upatikanaji wa nyama iliyo salama kwa walaji.
Amesema kuwa uwekezaji huo utasaidia kuchinja Mifugo mingi kwa muda mchache na kusambaza nyamba kwa walaji jambo litakaloongeza ajira kwa vijana na kukuza shughuli za kiuchumi.
Uboreshwaji wa Machinjio ya Ngelewala unatarajiwa kuifanya Iringa kuwa miongoni mwa maeneo yenye miundombinu bora ya machinjio nchini, sambamba na kuimarisha ushindani katika soko la nyama ndani na nje ya mkoa.