Nuru FM

Mwenyekiti akalia kuti kavu kwa ubadhilifu wa fedha

18 June 2026, 12:40

Mwenyekiti wa Sasa wa Mtaa wa Mjimwema akizungumza na wananchi. Picha Fredrick Siwale.

Na Fredrick Siwale

Wananchi wa Mtaa wa Mji Mwema mjini Mafinga wamemlalamikia aliyekuwa Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa huo kwa tuhuma za kuhujumu fedha zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya ununuzi wa vyombo vya msiba.

Mwenyekiti wa sasa wa Serikali ya Mtaa wa Mji Mwema, Ndg. Castor Nditu, amethibitisha kupokea malalamiko hayo na kudai kuwa juhudi za kufuatilia fedha hizo zinakwamishwa na baadhi ya viongozi wa CCM katika Kata ya Boma.

Sauti ya wananachi

Kwa mujibu wa Ndg. Nditu, aliyekuwa Mwenyekiti wa Mtaa huo, Ndg. Fidelis Kisoma, ambaye aliondolewa madarakani kutokana na tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka, anadaiwa kutumia vibaya kiasi cha Shilingi 200,000 zilizokuwa za ununuzi wa vyombo vya mtaa.

Amesema kuwa madai hayo yamekuwepo kwa takribani miaka mitatu sasa, na hadi mwaka 2026 fedha hizo bado hazijarejeshwa. Aliongeza kuwa jitihada za kuzidai zinakabiliwa na vikwazo kutoka kwa baadhi ya viongozi wa CCM wa Tawi la Mji Mwema na Kata ya Boma.

Sauti ya Mwenyekiti

Kwa upande mwingine, Ndg. Castor Nditu, aliwatuhumu baadhi ya viongozi wa chama hicho kwa kuendelea kumkingia kifua mtuhumiwa. Alidai pia kuwa amekuwa akitishiwa kuitwa mbele ya Kamati ya Maadili ya CCM Akiwemo Fredrick Barton Mwamakimbula kutokana na msimamo wake wa kufuatilia suala hilo.

Sauti ya Mwenyekiti

Awali, Mwenyekiti wa CCM Tawi la Mji Mwema, Ndg. Godfrey Mhagama, aliwaahidi wananchi katika mkutano wa hadhara kwamba angechukua hatua za kufuatilia na kuhakikisha fedha hizo zinapatikana kutoka kwa Ndg. Kisoma.

Katibu wa CCM Kata ya Boma, Fredrick Barton Mwamakimbula  amesema kuwa mtuhumiwa huyo aliitwa mbele ya Kamati ya Maadili ya CCM kuzungumzia changamoto hiyo huku akisisitiza kuwa hawakubaliani na hatua za awali zilizochukuliwa.

Sauti ya Katibu

Hata hivyo, tuhuma hizi ni madai yaliyotolewa na wananchi na viongozi husika, na mtuhumiwa hajatoa maelezo yake kuhusu tuhuma hizo.