Nuru FM

Wazee CCM Iringa walaani wanaobeza uwekezaji wa Bandari

3 August 2023, 8:00 pm

Miongoni mwa Wazee wa CCM mkoa WA iringa. Picha na Mpiga Picha Wetu

Na Frank Leonard

Wazee wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa wametangaza kuishiwa na uvumilivu na kuamua kulaani vikali mwenendo wenye viashiria vya kisiasa unaotishia kuigawa nchi kupitia matamko na maoni mbalimbali yanayotolewa kuhusu suala la uwekezaji wa bandari.

Pamoja na bandari, wazee hao wamesema wao pia ni sehemu ya Watanzania wanaounga mkono maridhiano ya vyama vya siasa yaliyoanzishwa na Rais Samia Suluhu Hassan lakini yatawafanya wasikae kimya na hata kutoa ushauri mgumu pale watakaposikia baadhi ya wanasiasa wakiyatumia kumdhihaki na kumkashfu Rais.

Kupitia tamko lao lililotolewa mjini Iringa leo na Mwenyekiti wa Wazee wa CCM Mkoa wa Iringa, Aman Mwamwindi mbele ya wawakilishi wa wazee wa kata zote 18 za mjini Iringa, wazee hao wamesema kwa nia njema Rais alitoa fursa kwa wananchi wake kutoa maoni kuhusiana na uwekezaji huo wa bandari.

“Inasikitisha kuona baadhi ya watu wamechukulia mjadala huu kwa dhamira za kuigawa nchi kikanda na kidini. Wazee tunakemea kwa nguvu zote tabia hii inayoweza kusababisha kuvunjika kwa Amani, utulivu, umoja na mshikamano wa nchi tuliorithi kutoka kwa waasisi wetu Mwalimu Julius Nyerere na Sheik Abeid Amani Karume,” amesema.

Mwamwindi amesema wazee wa mkoa wa Iringa wanawashauri watoa maoni watumie lugha ya staha huku wakijali uzalendo na sio maslai binafsi.

“Sisi wazee wa mkoa wa Iringa tupo pamoja na Rais Samia Suluhu Hassan na serikali yake na tunaunga na tutaunga mkono uwekezaji wowote ule ili mradi ufanyike kwa maslai ya Taifa letu,” amesema.

Kuhusu maridhiano ya kisiasa, wazee hao wamevitaka vyama vya siasa kupitia kauli mbalimbali zinazotolewa na viongozi au wanachama wao kuheshimu mamlaka ya Rais na kutumia lugha zinazoendana na hadhi hiyo ili kulinda, kuheshimu na kuiendeleza dhamira njema inayokusudiwa katika maridhiano hayo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa Daudi Yasin aliyehudhuria shughuli hiyo kama mwalikwa amesema wanachama na wapenzi wa CCM wa Mkoa huo wanaimba wimbo mmoja katika uwekezaji wa bandari wakiamini jambo hilo lina nia njema na litakuwa na manufaa makubwa kwa maendeleo ya Taifa.

“Serikali imeamua kuwekeza katika jambo hili, kwa ufafanuzi na elimu inayoendelea kutolewa kuhusu uwekezaji huu hatuna mashaka kwamba jambo hili lina nia njema. Tusiwasikilize watu wanaopotosha,” amesema.