Nuru FM

Wizara ya Afya Yawajengea uwezo Wanahabari Iringa.

11 July 2023, 5:45 pm

Afisa Program ya chanjo wa mpango wa Taifa wa chanjo kutoka Wizara ya Afya Lotalis Gadau Akitoa maelekezo kwa Wanahabari. Picha na Adelphina Kutika

Na Adelphina Kutika

Wizara ya Afya imeendelea kuwajengea uwezo Waandishi wa Habari nchini kuhusiana na masuala ya chanjo ili waweze kuelimisha jamii.

Afisa Program ya chanjo wa mpango wa Taifa wa chanjo kutoka Wizara ya Afya Lotalis Gadau amesema Wizara ya Afya imeendelea kutoa chanjo mbalimbali zikiwemo za surua kwa watoto na saratani ya shingo ya kizazi kwa watoto walio chini ya miaka kumi na nne.

Aidha amesema watatoa mafunzo kwa wanahabari katika Kanda zote na Zanzibar ili kuzuia maradhi mbalimbali na vifo.

Hata hivyo ametoa rai kwa maafisa wa chanjo katika mikoa yote nchini kutoa ushirikiano kwa Waandishi wa Habari ili elimu iweze kuwafikia wananchi badala ya urasimu usio na tija.

Baadhi ya Wanahabari wakifuatilia kwa umakini mafunzo. Picha na Adelphina Kutika

“Namshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutenga pesa kila mwaka kwa ajili ya chanjo mikoa yote nchini”alisema Gadau.

Hans Mapunda ni Mratibu wa chanjo Mkoa wa Iringa amesema Mkoa wa Iringa kama mikoa mingine inatoa chanjo mbalimbali zikiwemo za watoto, wasichana walio chini ya miaka kumi na nne na ya kuzuia pepo punda kwa wajawazito pia kwa wanawake wenye umri wa kuzaa.

Katika hatua nyingine Mapunda amesema kwa kushirikiana na watoa huduma kwa jamii huwatafuta watoto wasiopatiwa chanjo na wakiwabaini huwafikisha vituo vya chajo na kuwachanja wakiwemo jamii ya wafugaji ambao wamekuwa na tabia ya kuhama.

Amesema wameweka mkakati kuhakikisha makundi yote yamepata chanjo wakiwemo wasichana waliopata chanjo ya kwanza shule za msingi na sekondari na kwamba hawana uhaba wa chanjo.

Clensensia Kapinga amesema mafunzo waliyoipata yatasaidia kuondoa dhana potofu iliyojengeka kuwa ukichanjwa utakuwa mgumba.

Kwa upande wake Joachim Nyambo amesema Waandishi pamoja na wataalam watafanya uchechemzi wa masuala ya chanjo ili kupata matokeo chanya yatakayo punguza kama si kuyamaliza matatizo ya magonjwa kwenye jamii.

Kupitia mafunzo hayo Waandishi wataandaa vipindi vya kuelimisha jamii ili waone umuhimu wa chanjo.