Nuru FM

Rais Samia Kuanza Ziara Ya Kiserikali Nchini Uganda

10 May 2022, 7:36 am

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan anatarajia kufanya Ziara ya Kiserikali ya siku mbili nchini Uganda kuanzia tarehe 10 – 11 Mei, 2022 kwa mualiko wa Mhe. Yoweri Kaguta Museveni, Rais wa Jamhuri ya Uganda.

Hii itakuwa ni Ziara ya kwanza ya Kiserikali nchini kufanywa na Rais Samia tangu Serikali ya Awamu ya Sita iingie madarakani mwezi Machi 2021.

Madhumuni ya ziara hiyo ni kuimarisha na kudumisha zaidi historia iliyopo na mahusiano ya kidiplomasia pamoja na ushirikiano wa kiuchumi na kijamii kati ya nchi hizo mbili.

Katika ziara hiyo, Wakuu hao wawili wa Nchi na Serikali wanatarajiwa kujadili kuhusu masuala ya nishati, biashara, usafiri, maendeleo ya miundombinu pamoja na sekta za afya.