Nuru FM

Iruwasa kutoa elimu maadhimisho ya wiki ya maji Iringa

18 March 2024, 12:58 pm

Afisa uhusiano kutoka Iruwasa akizungumzia kuhusu wiki ya Maji katika Kipindi Cha Nyambizi Nuru FM. Picha na Oppa Chogga.

Iringa ikiadhimisha wiki ya maji, Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira IRUWASA imepanga kuhakikisha huduma ya maji inawafikia wananchi wote.

Na Hafidh Ally

Ikiwa tupo katika wiki ya maji, Mamlaka ya maji na usafi wa mazingira IRUWASA Mkoa wa iringa imeanza kutoa elimu kwa uma kuhusu matumizi bora ya huduma hiyo.

Akizungumzia kuhusu maadhimisho hayo, Afisa mahusiano kutoka Iruwasa Bi Restituta Sakila amesema kuwa watakuwa wakitoa elimu na semina kwa watumishi wa umma sambamba na kupokea ushauri kuhusu utoaji wa huduma ya maji kwa wananchi.

Bi Sakila amesema kuwa watoa huduma wana jukumu la kuhakikisha huduma ya maji inawafikia wananchi wote kwa ufanisi.

Wizara ya Maji imekuwa ikiratibu wiki ya maji kitaifa kila mwaka hapa nchini kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali wa sekta ya maji ambapo Maadhimisho haya yanatokana na Azimio Na. 47/193 la Umoja wa Mataifa (UN) kuwa kila ifikapo Machi, 22 ya kila mwaka nchi wanachama ziadhimishe Siku ya Maji Duniani kwa pamoja.