Nuru FM

MSD yapongezwa kwa kukabidhi vifaa tiba katika vituo vya Afya mkoani Tanga

17 July 2022, 1:39 pm

SERIKALI kupitia Bohari ya Dawa (MSD) imepongezwa kwa kuwezesha kukabidhi vifaa tiba katika vituo vya afya mkoani Tanga, vifaa ambavyo vilikuwa changamoto katika utoaji huduma vituoni humo.

Akizungumza leo Julai 17,2022 katika mahojiano maalumu Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Makorora mkoani Tanga, Dkt.Angelina Meshack amesema walipokea vifaa vya chumba cha upasuaji ikiwemo kitanda cha upasuaji, mashine ya dawa ya usingizi na taa zinazotumika wakati wa upasuaji amesema vifaa hivyo ni msaada mkubwa katika kituo hicho kwani awali kulikuwa na changamoto kwenye hutoaji huduma.

“Awali tulikuwa hatufanyi upasuaji kabisa kwa hiyo tulivyopokea fedha kwa ajili ya ukarabati majengo ya kufanyia upasuaji tulifanya hivyo na baadae vifaa vililetwa na MSD na kuanza kutoa huduma za upasuaji”. Amesema Dkt.Angelina

Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Makorora mkoani Tanga, Dkt.Angelina Meshack akizungumza na baadhi ya watumishi wa MSD mara baada ya kutembelea kituo cha afya cha Makorora kilichopo mkoani Tanga

Amesema baada ya kukabidhiwa vifaa hivyo walianza kutoa huduma ya upasuaji mbalimbali wa mama wajawazito pamoja na upasuaji mdogo kwani hapo awali walikuwa wanawapeleka wagonjwa hospitali ya Bombo kwa sababu huduma hiyo haikuwepo hapo kituoni.

“Kwa ujio wa vifaa hivi imerahisisha mama mjamzito akipata changamoto  moja kwa moja tunaweza kumpa huduma ya upasuaji na tunaokoa maisha ya mama pamoja na kichanga”. Amesema.

Pamoja na hayo Dkt.Angelina amesema walikabidhiwa pia na jenereta kwa ajili ya hospitali hiyo lakini wakaamua kuwasiliana na ofisi ya mganga mkuu ili waweze kuichukua na kuikabidhi kwenye vituo vingine ambavyo havina jenerata kwa sababu kituo hicho kilikuwa na jenerata ambayo walikuwa wameshanunua awali.

Ameeleza kuwa hali ya upatikanaji wa dawa katika kituo hicho ni nzuri kwani kwa sasa dawa muhimu zinapatikana kwa asilimia 90 na wanaendelea kutoa huduma bora kwa wananchi .

Naye Mfamasia wa Kituo cha Afya Ngamiani mkoani humo, Bw. Michael Mrosso amesema walipokea vifaa tiba kwa aajili upasuaji pamoja na jenerata, vifaa ambavyo vilikuwa ni kilio chao kwa muda mrefu.

Amesema wataendelea kujitahidi kutoa huduma bora kwa kuwa kuna vifaa bora ambavyo wamekabidhiwa na serikali kwa ajili ya kuwahudumia wananchi