Nuru FM

Wananchi Wa Chiwana Na Umoja Waipongeza Serikali Kutimiza Ahadi Ya Maji

15 March 2022, 8:00 am

WANANCHI wa kijiji cha Chiwana na Umoja kata ya Chiwana wilaya ya Tunduru,wameishukuru Serikali kwa kutimiza ahadi ya kuwapatia huduma ya maji safi na salama na kumaliza tatizo  la miaka mingi la wananchi  hao kutumia maji ya visima vya asili ambayo hayakuwa salama  kwa matumizi yao.

Wametoa kauli hiyo  kwa nyakati tofauti, wakati wakizungumza na baadhi ya waandishi wa Habari  wa mkoa wa Ruvuma waliofika katika vijiji hivyo kwa ajili ya kuangalia ujenzi wa mradi mkubwa wa  maji uliotekelezwa na  wakala wa maji  na usafi wa mazingira (Ruwasa)wilaya ya Tunduru ambao utahudumia wakazi  4,000.

Walisema, kufikishwa kwa maji ya bomba katika makazi yao imesaidia sana kumaliza changamoto hiyo  iliyowatesa kwa mrefu na ambayo  ilikwamisha kushindwa  kushiriki kazi za kiuchumi.

Jemshid Hamis  wa kijiji cha Chiwana alisema,wanawake wa kijiji hicho  ndiyo walikuwa waathirika wakubwa wa tatizo la ukosefu wa maji safi na salama kwa kuwa walilazimika kuamka mapema alfajiri kati ya saa 10 na 11 kwenda kusaka  huduma ya  maji.

Alisema, hata baadhi ya wanawake ndoa zao zimevunjika  kwa sababu ya kutumia muda mrefu pindi wanapokwenda kutafuta  maji ambayo yanapatikana kwenye visima vya asili na kushindwa kurudi haraka nyumbani kutokana na  umbali na changamoto mbalimbali wanazokutana nazo.

Aidha alisema, kero ya maji imesababisha  umaskini mkubwa,kwa kuwa wakati mwingine wanakosa muda wa kufanya kazi  mbalimbali za maendeleo, badala yake wanatumia muda huo kutafuta maji.

Mayasa Bakari mkazi wa kijiji cha Umoja alisema,kabla ya kufika kwa mradi huo walikabiliwa na changamoto nyingi ikiwamo magonjwa ya matumbo na kuhara kwa sababu ya kutumia maji ambayo sio safi na salama.

Alisema,baada ya kukamilika kwa mradi sasa wamepata faraja na matumaini makubwa kwani tangu ulipoanza kufanya kazi umemaliza kabisa tatizo la maji safi na salama ambapo  sasa wananchi wanapata fursa ya kufanya shughuli za uzalishaji mali.

Kwa upande wake Mganga wa Zahanati ya Chiwani Jenifer Valentino alisema, kabla ya kujengwa kwa mradi wa maji safi na salama,changamoto kubwa kwa wakazi wa kijiji hicho ilikuwa  magonjwa ya kuhara na matumbo mara kwa mara kutokana na kutumia maji ya visima vya asili ambayo hayakuwa salama.

Kwa mujibu wake, sasa idadi ya watu wanaofika katika zahanati hiyo kwa ajili ya kupata matibabu kutokana na kusumbuliwa na maradi hayo imepungua  kwa kiwango kikubwa.

Amewashauri wananchi wa kijiji hicho, kuendelea kutumia maji ya bomba ambayo ni  safi na salama kwa matumizi yao ya kila siku, badala ya kuendelea kutumia maji ya visima vya asili.

Naye Fundi Sanifu wa Ruwasa wilaya ya Tunduru Kassim Dinny alisema,mradi wa maji Chiwana ni kati ya miradi  iliyotekelezwa kupitia mpango wa lipa kutokana na matokeo(P4R) kwa kuwatumia wataalam wa ndani.

Alisema,mradi maji Chiwana unahudumia  vijiji viwili vya Chiwana na Umoja ambapo jumla ya wakazi wanaonufaika ni 4,281  na umegharimu jumla ya Sh. 182,531,648.88.

Alisema, kati ya fedha hizo Serikali kuu imetoa Sh.175,996,148.88,nguvu za wananchi Sh.6,535,500.00 ambapo mradi huo umetumia  fedha zote zilizotengwa na Serikali,na Sh.14,036,567.72 zimeokolewa na kutumika katika kazi za nyongeza.

Kassim alitaja kazi zilizoongeza ni pamoja na kuongeza mtandao wa bomba umbali wa mita 1,265 na kufanya jumla ya mtandao wa bomba wenye urefu wa mita 4,765 na kujenga vituo vingine vinne vya kuchotea maji.