Nuru FM

Mbunge KABATI Asisitiza Kutumia Michezo Ya Mabunge Afrika Mashariki Kuleta Amani

27 November 2022, 7:45 am

Mbunge wa viti maalum mkoa wa Iringa, Dkt. Ritta Kabati ametoa wito kwa nchi za Jumuiya Ya Afrika Mashariki kuitumia michezo ya mabunge ya Jumuiya hiyo kuleta amani kwa nchi za Jumuiya Afrika Mashariki zenye migogoro ya kisiasa.

Kabati ameyasema hayo akiwa Juba nchini Sudan Kusini kwa ajili ya kushiriki michuano iliyozinduliwa rasmi siku ya tarehe 25 Novemba, 2022, Mjini Juba.

Amesema kutokana na uwepo wa wabunge kutoka katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ni rahisi zaidi kupaza sauti ya kuleta amani katika maeneo yenye migogoro.

Dkt. Kabati ameongeza kuwa amani katika maeneo yenye migogoro itasaidia watoto kupata haki zao za msingi pamoja na kupunguza visa vya ukatili wa kijinsia kwa wanawake vinavyotokana na migogoro katika jamii.

Aidha Dkt. Kabati amepongeza ushiriki wa nchi wa wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuonesha huku akitamba timu ya Bunge Sports kutoka bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuibuka kidedea kwa kubeba vikombe vingi msimu huu.

Kauli Mbiu ya michezo hiyo ni Kupanua na Kuimarisha Muungano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kuongeza umoja wa Wananchi wake kupitia michezo.