Nuru FM

TANESCO Yaendeleza Jitihada Kukabiliana Na Hali Ya Upungufu Wa Umeme Nchini

16 December 2022, 4:54 pm

Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), limefanikiwa kupunguza makali ya upungufu wa umeme kutoka wastani wa megawati 350 kwa wiki zilizopita hadi kufikia wastani wa megawati 150 kwa sasa.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco Bw. Maharage Chande mbele ya waandishi wa habari jijini Dar es salaam alipokuwa akitoa taarifa juu ya jitihada zinazoendelea kufanyika ili kukabiliana na hali ya upungufu wa umeme nchini.

Bw. Chande ameeleza kuwa mpaka sasa wamefanikiwa kuongeza megawati 90 za umeme kwenye Gridi ya Taifa baada ya kukamilika kwa majaribio ya mitambo miwili ya gesi iliyopo katika kituo cha upanuzi wa kinyerezi namba 1

“Tuliahidi kwamba kuna marekebisho tutawahisha ili tuongeze megawati kwenye gridi zinazotumia gesi kama hatua za muda mfupi ambazo tulizungumza zikiwamo kuharakisha matengenezo na ufungaji wa mitambo, napenda kutoa taarifa kwamba kwenye hizo kazi za vituo vya gesi za muda mfupi nyingi zimekamilika kasoro moja na hivyo zimetuwezesha kupata hizo megawati tulizoahidi kwa kipindi cha muda mfupi na ndo maana mtaona katika siku za karibuni makali yale ya mgao yameanza kupungua”. Amesema Bw. Chande

Aidha majaribio ya mtambo mmoja uliopo katika kituo cha ubungo namba III wenye uwezo wa kuzalisha megawati 20 za umeme kwenda kwenye gridi ya taifa umekamilika lakini pia Tanesco wamefanikiwa kuwasha mtambo mmoja uliopo katika kituo cha upanuzi cha kinyerezi I tangu siku ya jumanne ya tarehe 13 Disemba na marekebisho mengine yanaendelea Hali itakayopelekea mtambo huo kuzalisha megawati 45 za umeme kwenda kwenye Gridi ya Taifa ifikapo wiki ya kwanza ya mwezi Januari 2023.

Ameeongeza kuwa, Mvua zinazoendelea kunyesha bado hazijawa nyingi za kutosha kuweza kuongeza kiwango cha uzalishaji umeme katika mabwawa ambapo mpaka sasa kituo cha New Pangani Falls(NPF) kinazalisha megawati 7 badala ya megawati 68, kituo cha Hale kinazalisha megawati 4 badala ya megawati 10.5, kidatu kinazalisha megawati 145 badala ya megawati 204 na bwawa la Nyumba ya Mungu linazalisha megawati 4 badala ya megawati 8.

Katika jitihada za muda mrefu zitakazofanyika shirika linategemea mtambo mwingine mmoja uliopo katika kituo cha upanuzi cha Kinyerezi namba I kuanza kufanya kazi ifikapo tarehe 8 Februari 2023 na utakuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 45 za umeme kwenda kwenye Gridi ya Taifa