Nuru FM

PSSSF yapewa siku 100 kukamilisha ujenzi kiwanda cha ngozi

22 February 2024, 7:46 pm

KATIBU Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhandisi Cyprian Luhemeja akiteta jambo na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Wafanyakazi wa Umma (PSSSF)  Abdul-Razaq Badru.

Na Mwandishi wetu

KATIBU Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhandisi Cyprian Luhemeja ametoa siku 100 kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Wafanyakazi wa Umma (PSSSF)  Abdul-Razaq Badru kuhakikisha awamu ya pili ujenzi wa kiwanda cha kuchakata bidhaa za ngozi Kilimanjaro unakamilika na kuanza kufanya kazi ifikapo Julai mwaka huu.

Agizo hilo amelitoa leo Februari 22, 2024 alipofanya ziara ya kukagua ujenzi katika kiwanda cha bidhaa za Ngozi Kilimanjaro International Leather Industries Ltd (KLICL) ikiwa ni sehemu ya kukagua maendeleo ya miradi inayotekelezwa na serikali kupitia ofisi hiyo.

Mhandisi Luhemeja amesema kukamilika kwa kiwanda hicho kutaongeza thamani ya zao la ngozi ghafi, kufungua fursa za soko la uhakika la ngozi kutoka kwa wafugaji, kuongeza ajira kwa vijana na mapato ya fedha za ndani na za kigeni.

Aidha, amefurahishwa na ubora wa bidhaa zinazozalishwa kiwandani hapo na kutoa wito kwa watanzania kuwa na tamaduni za kuthamini bidhaa zinazo zalishwa nchini.

Awali, akizungumza Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF,  Abdul-Razaq Badru amesema amepokea maagizo hayo ya Katibu Mkuu Mhandisi Luhemeja na kuahidi kuwa PSSSF kwa kushirikiana na Jeshi la Magereza watahakikisha wanafanya kazi kwa weledi kama ilivyo elekezwa ili watanzania waanze kunufaika na mradi huo.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda hicho, Mhandisi Saiba Edward amesema mradi huo pamoja na mambo mengine, utaongeza kipato kwa wakazi wa Kilimanjaro na mikoa jirani kupitia fursa za uzabuni, uwakala na usambazaji wa bidhaa.