Miundombinu bora yaongeza mahudhurio ya wanafunzi
23 June 2026, 16:31

Na Adelphina Kutika
Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI imesema kuwa uboreshaji wa miundombinu ya vyoo katika shule mbalimbali nchini umechangia kwa kiasi kikubwa kuboresha mazingira ya kujifunzia na kuongeza mahudhurio ya wanafunzi, hususan wasichana.
Kauli hiyo imetolewa na mgeni rasmi wa mkutano wa Maafisa Elimu wa Sekondari kutoka wilaya 33 zinazotekeleza programu za Shirika la Campaign for Female Education (CAMFED) Tanzania, Bw. Ignas Chonya kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, wakati wa ufunguzi wa mkutano huo uliofanyika katika Ukumbi wa Siasa ni Kilimo mkoani Iringa na kueleza kuwa Serikali inatambua mchango mkubwa wa CAMFED katika kusaidia watoto wanaotoka katika mazingira magumu kupata elimu na kuboresha mazingira ya kujifunzia kupitia uwekezaji katika miundombinu ya shule, ikiwemo vyoo.

Kwa upande wake, Mkuu wa miradi kutoka CAMFED Tanzania, Dominica Lyambo, amesema mkutano huo umeandaliwa kwa lengo la kutathmini utekelezaji wa miradi ya elimu katika wilaya mbalimbali hizo 33 na kujadili mbinu bora za kuhakikisha ufadhili unaotolewa unawafikia walengwa.
Baadhi ya Maafisa Elimu walioshiriki mkutano huo wameeleza kuwa ujenzi wa vyoo katika shule zao yameongeza usalama na faragha kwa wanafunzi, jambo lililosaidia kuimarisha ustawi wa mahudhurio na ufaulu wa wanafunzi.
Hata hivyo mkutano huo umewakutanisha maafisa elimu mikoa 10 kujadili mafanikio na changamoto za utekelezaji wa programu mbalimbali za CAMFED katika sekta ya elimu.
