Idydc Microcredit yawa Mkombozi kwa wajasiriamali Ifunda
15 May 2026, 15:08

“Mkopo kutoka IDYDC umesaidia kusomesha watoto na kukuza Biashara”
Na Hafidh Ally
Wananchi wa Kijiji cha Ifunda Wilaya ya Iringa wameishukuru Taasisi ya Utoaji Mikopo ya IDYDC Microcredit kwa kuwapatia Mikopo iliyowasaidia kuanzisha biashara na kujikwamua kiuchumi.
Wakizungumza na Nuru FM baadhi ya wananchi wa Kijiji hicho wamesema kuwa IDYDC imekuwa Mkombozi kwao, licha ya kukuza biashara zao, pia mikopo hiyo imewasaidia kusomesha watoto wao.
Aidha wananchi hao wamesema kuwa wamenufaika kwa kujikita katika kilimo huku wengine wakikiri kurudi kukopa kwa mara nyingine baada ya kuona manufaa waliyoyapata.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Taasisi ya Utoaji Mikopo ya IDYDC Kanda ya Ifunda Joackim Kisinini amesema kuwa wananchi wa Kanda hiyo wamenufaika kwani kabla ya kukopa wanawapa elimu ya namna ya kufanya biashara.
Naye Meneja wa IDYDC Microcredit Anisia Mwinuka amesema kuwa wameweka kiwango kwa wale wanaokopa kwa mara ya kwanza mkopo usiozidi laki tano sambamba na kuwapatia semina ya biashara.
IDYDC Microcredit ni Taasisi inayotoa mikopo kwa wajasiriamali wadogo na wakubwa ambayo iko katika eneo la Siasa ni Kilimo inalenga Kutoa huduma za kifedha zinazoweza kufikiwa kwa jamii ambazo hazijafikiwa vizuri nchini Tanzania ili kukuza uchumi na maendeleo endelevu.