Nuru FM

Wananchi Kalenga walalamikia gharama kubwa za vibali vya ujenzi

7 August 2026, 10:15

Mbunge wa Jimbo la Kalenga akizungumza na wananchi wa Ulanda. Picha na Hafidh Ally

Na Hafidh Ally

Wananchi wa Kata ya Ulanda, Jimbo la Kalenga, wameilalamikia Halmashauri kwa kutoza gharama ya shilingi 50,000 kwa ajili ya kibali cha ujenzi, wakisema kiwango hicho ni kikubwa na kinawazuia kujenga nyumba za kisasa.

Wakizungumza na Nuru FM, baadhi ya wananchi kutoka vijiji vya Mwambao na Weru walisema kuwa, pamoja na kuhamasishwa kujenga nyumba bora, wengi wao hushindwa kutekeleza azma hiyo kutokana na gharama kubwa ya kupata kibali cha ujenzi.

Wananchi hao walidai kuwa hata wanaofanya ukarabati wa nyumba za zamani zilizojengwa kwa tope na kuziboresha kwa kiwango cha kisasa hulazimika kulipa kiasi hicho cha fedha, jambo walilosema linaongeza ugumu wa kuboresha makazi yao.

Sauti ya Wananchi

Akizungumzia suala hilo, Mbunge wa Jimbo la Kalenga, Jackson Kiswaga, amesema kuwa Baraza la Halmashauri lina mamlaka ya kutunga sheria ndogondogo zinazolenga kuongeza vyanzo vya mapato kwa ajili ya kugharamia shughuli za maendeleo katika halmashauri.

Sauti ya Mbunge

Hata hivyo, Kiswaga amesema atafanya mazungumzo na Halmashauri ili kutafuta namna ya kupunguza gharama ya kibali cha ujenzi, akieleza kuwa kiwango cha sasa kinaonekana kuwa kikubwa kwa wananchi wenye vipato vya chini.

Sauti ya Mbunge

Alisisitiza kuwa lengo ni kuhakikisha wananchi wanapata mazingira rafiki ya kujenga na kuboresha makazi yao bila kubebeshwa mzigo mkubwa wa gharama.