Nuru FM

Kabati asikia kilio cha bei ya mbolea ya ruzuku

15 September 2026, 10:20

Mbunge Ritta Kabati akizungumza na wananchi wa Boma la Ngombe. Picha na Hafidh Ally

Mbolea za ruzuku zinalenga kuwasaidia wakulima kupunguza gharama za uzalishaji na kuongeza tija.

Na Hafidh Ally

Wananchi wa Kata ya Boma la Ng’ombe, Wilaya ya Kilolo, wameiomba Serikali kuchukua hatua za haraka kutatua changamoto ya upatikanaji wa mbolea za ruzuku, wakisema hali hiyo inakwamisha shughuli za kilimo katika eneo hilo.

Wakizungumza wakati wa ziara ya kikazi ya Mbunge wa Jimbo la Kilolo, Dkt. Ritta Enespher Kabati, wananchi hao wamesema baadhi ya wakulima wanalazimika kununua mbolea kwa bei ya zaidi ya shilingi laki moja, hali wanayodai ni kinyume na utaratibu wa bei elekezi.

Sauti ya Wananchi

Akijibu changamoto hiyo, Mbunge wa Jimbo la Kilolo, Dkt. Ritta Enespher Kabati, amewataka wananchi kutoa taarifa na kuwataja mawakala wa mbolea za ruzuku wanaokiuka bei elekezi iliyowekwa na Serikali, ili hatua zichukuliwe.

Sauti ya Mbunge Kabati

Dkt. Kabati amesema ushirikiano kati ya wananchi na Serikali ni muhimu katika kuhakikisha mfumo wa ruzuku unawanufaisha wakulima waliokusudiwa, akisisitiza kuwa kuwatoza wakulima bei zisizo halali hakukubaliki.

Sauti ya Mbunge Kabati

Aidha, amewataka wananchi kuwa makini na kuhifadhi vielelezo vya manunuzi, ikiwemo risiti, ili kurahisisha ufuatiliaji na uchukuaji wa hatua dhidi ya mawakala watakaobainika kukiuka taratibu.

Katika ziara hiyo, wananchi wa Kata ya Boma la Ng’ombe walipata fursa ya kueleza changamoto mbalimbali zinazowakabili, huku Dkt. Kabati akiahidi kuendelea kuzifanyia kazi kwa kushirikiana na Serikali na mamlaka husika.