Iringa kupambana na vishoka wa mbegu feki
25 August 2026, 10:24

Matumizi ya mbegu bora kutoka ASA yanaweza kuwa chachu muhimu ya kuongeza uzalishaji na tija kwa wakulima.
Na Joyce Buganda
Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali kuwawezesha wakulima kupata mbegu bora za ruzuku, ikiwa ni sehemu ya kukabiliana na changamoto zinazowakabili wakulima na kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji Cha magozi kata ya ilolo mpya Diwani wa kata hiyo Patrick Muhegele wenye lengo la kutoa elimu katika kutumia mbegu bora amesema Serikali ya awamu ya 6 imesikia kilio kutoka kwa wakulima hivyo wanatakiwa kuandaa mashamba pamoja mbegu mapema.

Kwa upande wake Wakala Mkuu wa mbegu za serikali ASA chini ya Wizara ya kilimo na Mkurugenzi wa kampuni ya Mgongolwa Agrovet and Seeds Joseph Mgongolwa amesema mbegu hizi zimezalishwa zinamudu hali ya hewa yoyote kama mvua chache, mvua nyingi, mvua za wastani pia zinatunza unyevu mda mrefu na husifika kwa ubora wake na matokeo mazuri.
Mgongolwa amesema kata ya ilolo mpya Wana fursa kubwa katika kilimo Cha mpunga, alizeti na Mahindi hivyo mbegu hizo kutoka Wakala wa serikali ASA itakwenda kuwa muarobaini katika mavuno yenye tija kwao.
Kwa upande wao baadhi ya wakulima wa Kijiji hicho wamesema wanapata changamoto kubwa kutokana na kuletewa mbegu feki na kupelekea kujikuta wakipata matokeo hafifu hivyo ujio wa mbegu hizo utakwenda kuwasaidia kupata mavuno mazuri.
Awali Afisa kilimo wa kata ya Ilolo mpya Oswald Kapungu amesema kwa awamu hii serikali imejipanga kupambana na vishoka ambao wanawarubuni wananchi kwa kuwauzia mbegu feki kwa kuweka mawakala wa serikali Kila Kona akiwemo Mgongolwa Agrovet and Seeds CO LTD, kwa kusambaza mbegu za serikali chini ya Wizara ya kilimo (ASA).
