Nuru FM

Wananchi Mtwango kunufaika na jengo la mama na mtoto

28 July 2026, 10:28

Waziri Ulega akipokea taarifa ya utekelezaji wa Mradi wa Jengo la Mama na Mtoto Katika Kituo cha afya Mtwango. Picha na Hafidh Ally

Serikali inaendelea kuwekeza katika kuboresha miundombinu ya afya ili kusogeza huduma bora karibu na wananchi na kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma nchini.

Na Hafidh Ally

Zaidi ya wananchi 17,000 wanatarajiwa kunufaika na ujenzi wa jengo la huduma za mama na mtoto katika Kituo cha Afya Mtwango, Wilaya ya Mufindi, mkoani Iringa.

Wakiuzngumza na Nuru FM Baadhi ya wananchi wameeleza kuwa kukamilika kwa jengo hilo kutapunguza adha ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya, hususan huduma za mama na mtoto, hali itakayochangia kuboresha afya ya jamii.

Sauti ya Wananchi

Akikagua maendeleo ya ujenzi huo, Waziri wa Ujenzi ambaye pia ni Mlezi wa Mkoa wa Iringa, Abdallah Ulega, amemtaka mkandarasi kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati na kwa kuzingatia viwango vya ubora ili wananchi waanze kunufaika na huduma hizo mapema.

Sauti ya Waziri Ulega

Amesema kuwa Jengo hilo litakapokamilika linatarajiwa kutoa huduma za afya ya mama na mtoto, kupunguza wananchi kutembea umbali mrefu kupata huduma na kurahisisha upatikanaji wa huduma za uzazi kwa wakazi wa Kata ya Mtwango na maeneo jirani.

Mradi huo wenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 300 unalenga kuboresha huduma za afya kwa mama na mtoto, kupunguza vifo vinavyoweza kuzuilika vya akina mama na watoto, pamoja na kusogeza huduma muhimu za afya karibu zaidi na wananchi wa Wilaya ya Mufindi.