Shemdoe aziagiza Halmashauri kukuza vipaji vya michezo
10 June 2026, 08:58

“Ni vyema Halmashauri zikaweka mkakati wa kukuza na kutumia vipaji vitakavyopatika kupitia mashindano hayo kama fursa ya ajira“
Na Hafidh Ally
Halmashauri zote Nchini zimetakiwa kuweka mkakati wa kuanzisha na kuendeleza shule maalumu za kukuza vipaji vya michezo na sanaa zenye miundombinu rafiki na wataalamu ili kukuza vipaji vya vijana.
Hayo yamezungumzwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Profesa Riziki Shemdoe wakati wa ufunguzi rasmi wa Mashindano ya Umoja wa Michezo na Taaluma kwa Shule za Msingi Tanzania (UMITASHUMTA) na Umoja wa Michezo na Taaluma kwa Shule za Sekondari Tanzania (UMISETA) ambayo Kitaifa 2026 yanafanyika Mkoani iringa.

Prof. Shemdoe amesema kuwa michezo kwa sasa haipaswi kutazamwa kama michezo tu bali kama fursa kubwa na ajira za vijana huku akitolea mfano vijana wa timu ya taifa ya Tanzania chini ya Umri wa miaka 17 serengeti boys ambao wameweza kuiwakilisha nchi vyema katika michuano ya Afcon wakimaliza nafasi ya pili na kupata tiketi ya Kufuzu kombe la Dunia litakalofanyika huko Nchini Qatar.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Iringa Kheri James amesema kuwa Mkoa wa Iringa umejipanga kikamilifu kuwahudumia zaidi ya wageni na washiriki 10,000 wanaotarajiwa kushiriki katika mashindano ya UMITASHUMTA na UMISETA yanayoendelea kufanyika mkoani hapa.
Akitoa salamu za Mkoa wa Iringa, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Kheri James, amesema kuwa maandalizi yote muhimu yamekamilika na huduma zinazohitajika kwa wageni zinapatikana wakati wote ili kuhakikisha mashindano yanafanyika katika mazingira bora.
Naye naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI Bw. Atupele Mwambene amesema kuwa mashindano hayo yanaingia mwaka wa 52 toka kuanzishwa kwake yanalenga kukuza vipaji sambamba na kuendeleza Michezo na sanaa.
