Nuru FM
Nuru FM
16 April 2026, 08:09

Uchunguzi wa kitabibu ulithibitisha kuwa taarifa hizo hazikuwa za kweli na watuhumiwa hao wamefikishwa mahakamani.
Na Hafidh Ally
Jeshi la Polisi mkoani Iringa, limemkamata Ramadhani Mussa (53), dereva na mkazi wa Dar es Salaam, kwa kosa la kutoa taarifa za uongo kwamba ameibiwa sehemu zake za siri.
Taarifa hiyo imetolewa leo na Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Iringa, SACP Allan Bukumbi amesema kuwa baada ya uchunguzi kukamilika Ramadhani alifikishwa mahakamani, na hatimaye kuhukumiwa kifungo cha miaka mitano (5) jela kwa kosa hilo.
Kamanda Bukumbi amesema kuwa watuhumiwa Wengine ni Mussa Kaundi (39), mfanyabiashara wa Mafinga, pamoja na watuhumiwa wawili mmoja mkazi wa Isakalilo ndani ya Manispaa ya Iringa na mwingine wa Usokami, Mafinga ambao wanadaiwa kutoa taarifa za uongo kuhusu kuibiwa sehemu za siri.
Aidha Bukumbi amebainisha kuwa watuhumiwa wengine sita wamehukumiwa vifungo vya miezi mitatu hadi miaka mitatu kutokana na makosa mbalimbali ikiwemo kujeruhi, wizi, shambulio, kutishia kuua na uvunjaji.
Miongoni mwao ni Ernest Simagwa (44) aliyehukumiwa miaka mitatu jela kwa kujeruhi, na Baraka Nyamba (20) aliyepewa kifungo cha miezi sita kwa kosa la uvunjaji.
Kamanda Bukumbi ametoa onyo kwa wakazi wa Iringa na Watanzania kwa ujumla kuepuka kujihusisha na uhalifu au kusambaza taarifa za uongo, na badala yake kushirikiana na jeshi hilo ili kuhakikisha usalama unaimarishwa zaidi.