Nuru FM

CCM Iringa yaridhishwa na skimu ya umwagiliaji

16 July 2026, 09:21

Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Iringa Iikakgua skimu ya Umwagiliaji. Picha na Hafidh Ally

Mradi wa Skimu ya Umwagiliaji ya Mkombozi uliopo Tarafa ya Pawaga, Wilaya ya Iringa, utapanua eneo la umwagiliaji kutoka ekari 4,500 zilizokuwa zikitegemea mifereji ya asili hadi ekari 15,000, huku uzalishaji wa mpunga ukitarajiwa kuongezeka kutoka wastani wa tani mbili hadi tani tano kwa hekta kutokana na matumizi ya teknolojia na mbinu bora za kilimo.

Na Hafidh Ally

Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa imeridhishwa na utekelezaji wa Mradi wa Skimu ya Umwagiliaji ya Mkombozi uliopo Tarafa ya Pawaga, Wilaya ya Iringa, unaotekelezwa na Serikali kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 56.

Mradi huo, unaolenga kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo, kuimarisha usalama wa chakula na kuinua uchumi wa wananchi wa eneo hilo, umefikia asilimia 95 ya utekelezaji na unatarajiwa kukamilika pamoja na kukabidhiwa rasmi mwezi Septemba mwaka huu.

Akizungumza wakati wa ziara ya Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Iringa ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo wilayani humo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, Daud Yassin, amewataka wananchi kuwa walinzi wa miundombinu ya mradi huo kwa kuitunza na kuilinda ili idumu na kuendelea kuwanufaisha wananchi pamoja na vizazi vijavyo.

Sauti ya Daudi Yasin

Alisema Serikali imeanza pia kutatua changamoto zinazoweza kuhatarisha uwekezaji huo kwa kutenga maeneo maalumu ya kunyweshea mifugo ili kulinda miundombinu ya umwagiliaji, sambamba na kuendelea na zoezi la upimaji wa mashamba na utoaji wa hati za ardhi ili kuimarisha kilimo cha kisasa.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, amesema Serikali imewekeza katika ukanda wa Pawaga kupitia mradi huo wa umwagiliaji kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa chakula na kuimarisha usalama wa chakula nchini.

Sauti ya RC Kheri James

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Skimu ya Umwagiliaji Mkombozi, Chesco Msamba, amesema mradi huo umeleta matumaini mapya kwa wakulima kwa kuondoa changamoto ya utegemezi wa mifereji ya asili ya umwagiliaji, huku ukitarajiwa kuhudumia zaidi ya ekari 15,000 za mashamba.

Sauti ya Msamba

“Tulikuwa tunaanza upya kila mvua kubwa iliponyesha kwa sababu mifereji ilikuwa ikiharibika. Sasa tuna uhakika wa maji na tunaona mustakabali mpya wa kilimo chetu,” alisema.

Baadhi ya wananchi wanaonufaika na skimu hiyo wamesema mradi umeongeza fursa za kilimo cha uhakika, umewezesha uzalishaji wa mazao kwa mwaka mzima na kuboresha kipato pamoja na maisha yao kupitia shughuli za kilimo.

Sauti ya Wanufaika

Msindikaji wa mazao, Lukas Ndete, alisema ongezeko la uzalishaji limeongeza uwezo wa kiwanda chake kukoboa mpunga kutoka magunia 10,000 hadi kufikia magunia 27,000, hatua inayoongeza ajira na shughuli za biashara katika eneo hilo.