Vijana Kilolo watakiwa kutumia chuo cha Veta kujiajiri
14 July 2026, 09:42

Kamati ya Siasa Mkoa wa Iringa imekagua ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) Wilaya ya Kilolo kinachojengwa kwa gharama ya Sh bilioni 1.6 kupitia fedha za mapato ya ndani ya Serikali.
Na Hafidh Ally
Vijana Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo, wametakiwa kuitumia kikamilifu fursa ya Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) kinachojengwa na Serikali kwa gharama ya shilingi bilioni 1.6 kwa lengo la kupata ujuzi utakaowawezesha kujiajiri na kuajiri wengine, badala ya kuendelea kutegemea ajira za Serikali pekee wakati wote.
Akizungumza wakati wa ukaguzi wa mradi huo wa VETA unaojengwa katika Kijiji cha Luhindo kata ya Mtitu wilaya ya Kilolo, MwenyeKiti wa CCM Mkoa wa Iringa, Daudi Yassin akiwa ameambatana na wajumbe wengine wa kamati ya siasa kukagua utekelezaji wa ilani ya Uchaguzi mkuu 2025-2030, amesema kukamilika kwa chuo hicho ni fursa kwa vijana na wananchi wa wilaya hiyo.
Akizungumza baada ya ukaguzi huo, Yasin alisema wajumbe wa kamati wameridhishwa na ubora wa miradi hiyo na kusisitiza kuwa wananchi wana wajibu wa kuitunza ili iendelee kutoa huduma kwa muda mrefu.
Alisema Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika sekta ya elimu kwa kujenga shule mpya, mabweni, maabara na vyuo vya ufundi, hatua inayopanua fursa za elimu na kuwawezesha vijana kupata maarifa na ujuzi utakaowasaidia kujiajiri na kuajiriwa.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, amesema ujenzi wa Chuo hicho utasaidia vijana kupata ujuzi katika fani mbalimbali ambazo zitapelekea vijana kuwa na njia nyingi za kujiongezea kipato.
Kwa mujibu wa taarifa iliyowasilishwa na Afisa Udhibiti Ubora wa Shule Wilaya ya Kilolo, Alto Kinunda chuo hicho kinatarajiwa kukamilika Septemba 30, 2026 na kitapokea wanafunzi wapatao 240 katika fani mbalimbali za ufundi.
Kwa upande wake Katibu wa Itikadi, Siasa, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa Mkoa wa Iringa Joseph Nzala Ryata amesema kuwa chuo hicho kitasaidia vijana kupata ujuzi na kupunguza wimbi la vijana wasiokuwa na shughuli mtaani.
Hadi kufikia Julai 9 mwaka huu Serikali imepeleka Sh Milioni 777.4 kwa ajili ya mradi huo, ambapo zaidi ya shilingi milioni 608 zimetumika na ujenzi umefikia asilimia 76 ambao unahusisha ujenzi wa majengo tisa, yakiwemo jengo la utawala, madarasa matatu, karakana za useremala, uashi, umeme na ufundi bomba, ushonaji na upishi, jengo la umeme, nyumba ya mtumishi, jengo la mlinzi pamoja na vyoo vya jumuiya.
