Nuru FM

Kutokunywa maji chanzo cha ugonjwa wa mawe kwenye figo

7 June 2024, 12:18 pm

Picha ya muonekano wa figo ya binadamu.

Kwa mujibu wa utafiti wa hivi karibuni wa Shirika la India la Nephrology, watu milioni 84 duniani kote wanaugua magonjwa mbalimbali ya figo.

Na Mwandishi wetu

Jamii wilayani Mufindi imetakiwa kunywa maji mengi na kupunguza matumizi makubwa ya protini ili kuepukana na ugonjwa wa mawe kwenye figo.

Wito huo umetolewa na daktari wa mwili wa binadamu kutoka kituo cha afya Ifwagi Dkt. Chrsitopher Nicodemus Sengi na kuongeza kuwa ulaji mpitilizo wa protini husababisha binadamu kupata ugonjwa wa mawe kwenye figo.

Aidha Dkt. Sengi amesema kuwa ugonjwa huo unaathiri watu wa rika lote kwenye jamii na kwa sasa unashika kasi kubwa miongoni mwa vijana na wazee.

Nao baadhi ya wananchi katika Mji wa Mafinga wamekuwa na uelewa tofauti juu ya ugonjwa huu wa mawe kwenye figo na kuwaomba wataalamu waendele kutoa elimu kwa ajamii.

Ugonjwa wa mawe kwenye figo ni miongoni mwa magonjwa ya figo ambayo kwa binadamu husababisha madhara ikiwemo kifo na figo kushindwa kufanya kazi huku jamii ikishauriwa kunywa maji lita 2 mpaka 3 kwa siku, kutokula chumvi nyingi sambamba na kula matunda na mbogamboga.