Nuru FM

Lindi yakumbwa na ugonjwa wa ajabu

12 July 2022, 4:42 pm

Rais Samia Suluhu Hassan amesema kuna maradhi mapya ambayo yamezuka mkoani Lindi na kila wakati mapya yanaibuka wakati huko nyuma hayakuwepo.

Rais Samia ameyasema hayo leo alipokuwa akifungua Mkutano wa 20 wa Shirikisho la Baraza la Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati (Amecea) unaofanyika jijini Dar es Salaam katika ukumbi wa JNICC.

Rais Samia ametaja Mkoa wa Lindi kama moja ya maeneo ambayo magonjwa mapya yanaibuka na amepata taarifa kutoka kwa Waziri Mkuu.

“Kuna kila aina ya maradhi mapya yanazuka ambayo hatuyajui, nilikuwa nazungumza na Waziri Mkuu juzi ametoka ziara kule Mikoa ya Kusini, Lindi ameniambia ameona kuna maradhi mapya yameingia, Wanadamu wanatokwa tu damu puani na wanadondoka,” amesema Rais Samia.

Rais Samia amesema viumbe ambavyo vilipaswa kubaki misituni sasa vinasambaa kwa wanadamu kwa sababu ya uchafuzi wa mazingira na amewakumbusha watanzania kuhusu umuhimu wa kuhifadhi mazingira.

“Hatujui ni kitu gani ila Wanasayansi na Wataalamu wa Afya wote wamehamia huko wanaangalia ni kitu gani?, kwanini Mwanadamu atokwe tu na damu za pua adondoke, angekuwa mmoja wawili tungesema Presha imepanda vein zimepasuka anatokwa damu za pua lakini ni wengi kwa mfululizo ni maradhi ambayo hatujawahi kuona,” ameongeza Rais Samia.

Amesema mambo mengi yanaibuka kwa sababu ya uharibifu wa misitu.

“Yote ni kwasababu tunaharibu makazi ya viumbe kule walikoumbwa na Mungu, tunawasogeza kwetu wanatuletea aina yote hiyo ya maradhi.” Rais Samia.

Katika kuongelea usafi wa miji na majiji, Rais Samia amesema Mkoa wa Dar es Salaam umetangazwa kuwa Jiji la sita kwa usafi Barani Afrika.