Nuru FM

Acheni kwenda na watoto kilabuni

7 March 2024, 4:10 pm

Viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa na Jeshi la Polisi wakiwa katika maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani. Picha na Joyce Buganda.

Utaratibu wa wazazi kwenda na watoto Vilabuni chanzo Cha ongezeko la Ukatili dhidi ya watoto Mkoani Iringa.

Na Joyce Buganda

Mkuu wa Dawati la jinsia na watoto Mkoa wa Iringa Mkaguzi wa Polisi, Elizabeth Swai amewaasa Wanawake kuacha tabia ya kwenda kwenye vilabu vya pombe na watoto wao kwani kwa kufanya hivyo wanaharibu makuzi ya watoto na kutengeneza kizazi kisichokuwa na maadili mema katika Jamii.

Elizabeth Swai ameyasema hayo Machi 06, 2024 wakati akizungumza na wananchi waliohudhuria katika kilele cha siku ya wanawake duniani iliyofanyika kiwilaya katika shule ya Sekondari Kalenga iliyopo Mkoani Iringa.

Swai amesema kuwa, Wanawake wanachangia kwa kiasi fulani kutoa malezi mabaya kwa watoto yanayopelekea mmonyoka wa maadili kwani kuna baadhi yao wanaingia na watoto hao vilabuni na maeneo mengine ya starehe jambo ambalo ni kinyume na malezi bora ya mtoto.

Aidha, amesisitiza juu ya kuripoti matukio ya ukatili ambapo amesema wahanga wa ukatili wa kijinsia kwa asilimia kubwa ni wanawake pamoja na watoto hivyo amehimiza kuwalinda na Vitendo hivyo.

“Kina mama waleeni watoto wenu kwa maadii mazuri msiende na watoto wenu vilabuni”, alisistiza Swai.

Aidha amewataka Wanawake kutumia fursa mbalimbali zinazopatikana katika jamii na kujishughulisha kufanya kazi ndogondogo za ujasiriamali ,ili kuheshimika katika jamii na ngazi ya familia.

STEVEN MHAPA ni mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya iringa ndiye alikuwa mgeni rasmi ambae alimuwakilisha mkuu wa wilaya ya iringa amewaasa wanawake kutumia majukwaa katika kukumbushana majukumu yao.

“Ili nyumba ili iwe vizuri ni lazima mwanamke asimame imara aslimia 75 za mafanikio kuwepo katika familia zetu yanachangiwa na mwanamke” Alisema Mhapa

Kwa upande wao wanawake wa wilaya ya Iringa kupitia risala yao kwa mgeni rasmi katika maadhimidhimisho hayo, wameipongeza serikali ya wilaya na mkoa kwa kuwezeshwa kupatiwa mafunzo mbalimbali ya kijasiriamali na mafunzo ya namna ya kupambana na matukio ya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia.

Maadhimisho ya siku ya wanawake kitaifa yatafanyika march 8 na kimkoa pia yatafika march 8 katika viwanja vya samora huku yakibebwa na kauli mbiu isemayo WEKEZA KWA WANAWAKE KUHARAKISHA MAENDELEO YA TAIFA NA USTAWI WA JAMII.