Nuru FM

Mtazamo hasi wapelekea wanawake kushindwa kununua kondom

28 November 2023, 7:10 pm

Na Mwandishi wetu

Mitazamo tofauti imekuwa ikijitokeza kwenye jamii zetu juu ya suala zima la mwanamke kununua kinga (kondomu) moja kati ya mitazamo hiyo ni kuona au kumchukulia mwanamke anayeenda kununua kinga kama moja kati ya wanawake ambao hawajatulia kwenye mahusiano yao.

mitazamo hii husababisha hata mwanamke mwenyewe kujishuku na kuona anayetakiwa kununua kinga ni mwanaume tu huku akisahau ya kwamba jukumu la kulinda afya ni la wote kwa maana ni jukumu la kwake mwenyewe pamoja na mwenza wake.

Watu mbalimbali wamezungumza kwanini jamii ina kuwa na mtazamo hasi pindi mwanamke anapokwenda kununua kinga lakini pia hali hiyo humfanya mwanamke kutojiamini na kutonunua kinga mara nyingi huwaachia wanaume kununua kinga.

Doreen ambae ni muuzaji wa kinga hizo amesema kondomu nyingi za kike haziuziki hii ikiwa na maana ya kwamba wanawake hawapendi kununua kinga hizo na sababu kubwa ikiwa ni uoga wa wanawake wenyewe kwamba jamii itamchukuliaje kwa kuanza na muuzaji mwenyewe.

Shania ni moja kati ya wanawake ambao nimezungumza nao anasema tamaduni za Kitanzania ndio kikwazo kikubwa kwa wanawake na mazoea pia kuwa wanaume ndio wanaopaswa kununua kinga huku akipendekeza jamii inapaswa kupewa elimu juu ya matumizi ya kinga na kuambiwa kwamba kila mmoja anapaswa kulinda afya yake.

Nelly mkazi wa Zizi la ng’ombe ameeleza juu ya faida za matumizi ya kinga kwa mwanamke huku akisema matumizi ya kinga yanamuepusha mwanamke na magonjwa ya zinaa pamoja na mimba zisizotarajiwa hivyo jamii inapaswa kuwa na uelewa huku akitaka kuwe na usawa kwenye jamii zetu ndio maana wanawake wanaonekana hawajatulia kwenye mahusiano yao.

Salima mkazi wa Kihodombi mkoani Iringa amesema jamii inaamini mwanaume kama ndio mwanzilishi wa kila kitu na ndio maana mwanamke hawezi kuomba tendo la ndoa kwa mwenzi wake hii inapelekea hata mwanamke kutokupata ujasiri wa kwenda kununua kinga.Huku akisema mila na desturi kandamizi ndizo zinazopelekea hali hiyo.

Wapo baadhi ya wanaume ambao wametoa mitazamo yao ni kwa namna gani anamchukulia mwanamke ambae anaenda kununua kinga.

Musa mkazi wa Viwengi amesema “hawezi kumchukulia vibaya mwanamke anayenunua kinga kwasababu hiyo ni kwa ajili ya mustakabali wa afya yake kwa kumkinga na magonjwa mbalimbali huku akisema watu wengine wamekuwa na dhana ya kwamba mwanaume ndio anapaswa kununua au kuandaa”.

Amir mkazi wa ipogolo amesema “wanawake wenyewe wanakosa ujasiri hata kama wanakuwa na kinga huwa hawasemi kwa kuogopa kuonekana ni viruka njia pamoja na kutaka kuwaridhisha wanaume kwa kutaka kuonekana hawana tabia zisizofaa bila kujua ile ni kwa ajili ya usalama wa afya zao”.Lakini pia wanawake wengine hawataki kutumia kinga wakati wa tendo huku akiongezea wanawake wanaouza miili yao ni salama zaidi kuliko wanawake wengine hii yote ni kutokana na umakini uliopo kati ya wanawake hao.

Juma Manota mkazi wa Donbosco amesema mwanamke ambae Ananunua kinga moja kwa moja ni mwanamke anayejitambua,anayejielewa na mwenye elimu na kuongeza kwamba wataalamu inabidi watoe elimu ya matumizi na umuhimu kinga kwa mfumo wa semina mbalimbali.

Bi Dostana ambaye ni Afisa Afya Manispaa ya Iringa ameelezea umuhimu wa kutumia kinga huku akisema “inamsaidia mwanamke pamoja na mwenzi wake kuwa salama dhidi ya magonjwa ya ngono lakini pia mwanamke anatoka katika hatari ya mimba zisizotarajiwa”. Lakini ameendelea kwa kusema “mwanamke anayepata ujasiri wa kwenda kununua kinga anatambulika kama mwanamke anayejitambua na kujali afya yake na hivyo kusisitiza kuwa wanawake waache uoga kwasababu hizo kinga zipo kwa ajili yao pia si kwaajili ya wanaume tu”.

Kwa mujibu wa takwimu mbalimbali zinaeleza kuwa baadhi ya mimba zisizotarajiwa zinasababishwa na dhana potofu juu ya matumizi ya kinga kwa wanawake. Huku maambukizi ya VVU kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zikionesha kupungua sana hadi kufikia mwezi Aprili mwaka 2023.