Nuru FM

ASAS kujenga kiwanda cha maziwa Njombe

16 August 2023, 10:39 am

Mkurugenzi wa Kampuni ya ASAS Diaries Iringa Ahmed Salim Abri akiwa na Mkuu wa Wilaya ya Njombe Kissa Kasongwa katika mashamba Yao. Picha na Hafidh Ally

Na Hafidh Ally

Kampuni ya Asas Diaries @asas_dairies Mkoani Iringa inatarajia kujenga kiwanda cha maziwa katika Wilaya ya Njombe ili kuwainua wafugaji wa eneo hilo na kukuza uchumi.

Hayo yamezungumzwa na Mkurugenzi wa Kampuni hiyo Ahmed Salim Abri @ahmed.s.asas mara baada ya kutembelewa na kamati ya Ulinzi na usalama Wilaya ya Njombe ambayo iliongozwa na Mkuu wa Wilaya hiyo Kissa Kasongwa na kuongeza kuwa kampuni yao imeonesha nia ya kuwekeza kiwanda cha kisasa.

Amesema kuwa wameongea na uongozi wa Wilaya ya Njombe ili wawapatie eneo ambalo watawatuma wataalamu wao na kufanya utafiti na kisha wataanza ujenzi wa kiwanda.

Tumewaalika viongozi hawa kuja kutembelea kiwanda chetu na kujionea fursa za uwekezaji katika mashamba yetu ya ASAS, tuna imani watakuwa wamejifunza mambo mengi ya uwekezaji na sisi tumeonesha nia ya kuwekeza mkoani Njombe kwa sababu tuna wafugaji wengi ambao tunanunua maziwa kutoka huko” alisema Ahmed

Aidha Amesema kuwa Kampuni yao imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha wanapunguza tatizo la utapiamlo katika mikoa ya Nyanda za juu kusini ambapo wamekuwa wakitoa maziwa katika shule za msingi.

“Tumekuwa tukitoa maziwa katika eneo la njombe shule ya msingi viziwi, na makambako ambapo tunatoa maziwa lita 120 za maziwa kwa siku ili kusaidiana na serikali katika mkakati wa lishe bora shuleni” alisema Ahmed Abri

Akizungumzia kuhusu Mradi wa TPI3 kwa kushirikiana na Benki ya Kilimo TADB, amesema kuwa Kampuni yao itatoa Mikopo ya Ng’ombe kwa wafugaji ambao wana kikundi kinachotambulika ili kuongeza tija ya uzalishaji wa maziwa.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Njombe Kissa Kasongwa amesema kuwa Ofisi yake iko tayari kutoa eneo Kwa Kampuni ya ASAS ili watekeleze ujenzi wa Kiwanda cha maziwa na kukuza uchumi wa wilaya hiyo.

“Ofisi yetu iko tayari kupokea fursa hii ya uwekezaji wa kiwanda na tutahakikisha Mnapata eneo na kulimiliki kihahalali ili muwekeze katika wilaya yetu ya njombe, tumeona pia mkiwekeza mtatoa mikopo ya Ng’ombe ( Mitamba) kwa wafugaji wetu” alisema Kissa

MWISHO