Nuru FM

Iringa yapaa Kimataifa uhifadhi wa Mazingira

18 December 2022, 12:41 pm

Meya wa Manispaa ya Iringa, Ibrahim Ngwada amesema Tanzania imepaa tena kimataifa baada ya mji wa Iringa kuorodheshwa kuwa ni mojawapo kati ya miji 15 Duniani, ambayo inazingatia usafi na utunzaji wa Mazingira.

Ngwada ameyasema hayo wakati akiongea na waandishi wa Habari ofisini kwake mjini Iringa, na kuwapongeza wananchi, wadau na Mamlaka za Serikali ya Mkoa wa Iringa kutokana na hatua hiyo huku akiwataka kuendeleza juhudi za ustawishaji, usafi na utunzaji wa Mazingira.

Amesema, tangazo la kutajwa kwa Manispaa ya Iringa kuwa na sofa hiyo, lilitolewa Desemba 12, 2022 nchini Canada, na hivyo kupewa cheti maalum cha utambuzi wa utambuzi wa Manispaa ya Iringa katika suala la usafi na utunzaji wa mazingira.

Ngwada ameongeza kuwa, “Mji wetu wa Iringa umetajwa sambamba na miji mingine ikiwemo Marekani yenye miji minne, Colombia yenye miji miwili, Canada yenye mji mmoja, Thailand ambayo mji wake mmoja umetajwa na pia nchi ya Uganda na Kenya ambazo kila moja mji wake mmoja umetajwa.”

Aidha, Meya Ngwada amesema Iringa sasa inaungana na miji mingine 256 zilizopo katika mataifa mbalimbali ulimwenguni, ambazo zimeorodheshwa kwa uzingatiaji huo wa usafi na utunzaji wa Mazingira na kusema hiyo ni fursa ya kutengeneza mtandao wa miji marafiki ili kubadilishana ujuzi katika nyanja za kimazingira.

Hata hivyo, amesema kupitia hatua hiyo in wazi kuwa watalii wataongezeka na kuongeza pato la Mkoa, Taifa na mtu mmoja mmoja kupitia biashara mbalimbali na kwamba Iringa sasa inakuwa na kioo kwenye suala la uhifadhi na utunzaji wa mazingira.